• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Sergio Ramos akubali kuchezea PSG kwa mkataba wa miaka miwili

Sergio Ramos akubali kuchezea PSG kwa mkataba wa miaka miwili

Na MASHIRIKA

SERGIO Ramos amekubali kujiunga na Paris Saint-Germain (PSG) kwa kandarasi ya miaka miwili na anatarajiwa kutia saini mkataba huo wakati wowote.

Beki huyo raia wa Uhispania sasa hana klabu baada ya Real Madrid aliowachezea kwa miaka 16 kutorefusha zaidi muda wa kuhudumu kwake ugani Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Mbali na PSG, vikosi vingine vilivyokuwa vikiwania huduma za Ramos ni Manchester City, Chelsea na Bayern Munich.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha RMC nchini Ufaransa, PSG tayari wameafikiana na Ramos ambaye alitua jijini Paris mnamo Juni 30 na akakutana na rais wa kikosi hicho, Leonardo Araujo ambaye alishiriki naye mazungumzo ya kina.

Ramos alichochewa kuondoka Real baada ya miamba hao wa Uhispania na bara Ulaya kukataa kumwongezea kandarasi mpya ya miaka miwili.

Hivyo, amehiari kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za PSG ambao kwa sasa watakuwa wakimpokeza mshahara wa Sh19 milioni mwishoni mwa kila wiki, hii ikiwa takriban nusu ya ujira aliokuwa akilipwa na Real Madrid uwanjani Santiago Bernabeu mwisho wa kila juma.

Neymar Jr aliyewahi kuchezea Barcelona ambao ni washindani wakuu wa Real nchini Uhispania, ni miongoni mwa wanasoka ambao wamechangia pakubwa kushawishi Ramos kuingia katika sajili ya PSG.

Angel Di Maria na Keylor Navas ambao waliwahi kucheza pamoja na Ramos kambini mwa Real sasa wanavalia jezi za PSG kwa pamoja na Ander Herrera, Pablo Sarabia, Sergio Rico na Juan Bernat ambao ni raia wa Uhispania.

PSG tayari wamejinasia huduma za kiungo Georginio Wijnaldum na kipa Gianluigi Donnarumma bila ada yoyote kutoka Liverpool na AC Milan mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Baada ya sare na Gor Mahia sasa Bandari FC yapania kuichapa...

NDONDI: Timu ya taifa yaimarisha maandalizi ya Olimpiki