• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Barcelona na Atletico Madrid nguvu sawa katika Ligi Kuu ya Uhispania

Barcelona na Atletico Madrid nguvu sawa katika Ligi Kuu ya Uhispania

Na MASHIRIKA

BARCELONA walipoteza fursa ya kutua kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumamosi baada ya kulazimishiwa sare tasa na viongozi wa jedwali Atletico Madrid uwanjani Camp Nou.

Matokeo hayo yaliwaweka nambari tatu Real Madrid katika nafasi nzuri zaidi ya kuhifadhi ufalme wa La Liga muhula huu iwapo watakung’uta nambari nne Sevilla mnamo Mei 9, 2021. Ushindi kwa Real utawapaisha hadi kileleni mwa jedwali ikizingatiwa kwamba wanajivunia rekodi nzuri dhidi ya Atletico ya kocha Diego Simeone.

Ingawa hivyo, kikosi chochote ndani ya mduara wa nne-bora kwa sasa kina uwezo wa kunyanyua ufalme wa La Liga muhula huu kutegemea jinsi matokeo ya kila timu yatakavyokuwa katika jumla ya mechi tatu zilizosalia kwenye kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Ingawa Barcelona walijituma vilivyo, walishindwa kupenya ngome ya Atletico waliocheza kwa kubana sana safu yao ya ulinzi japo Lionel Messi alimshughulisha kipa Jan Oblak mara kadhaa langoni.

Atletico nao walipata nafasi kadhaa za kufunga bao katika kipindi cha pili ila makombora ya Luis Suarez yakadhibitiwa vilivyo na kipa Marc-Andre ter Stegen.

Mnamo Januari, Barcelona walikuwa nyuma ya Atletico kwa alama 13 na kocha Ronald Koeman akakata tamaa ya kuongoza waajiri wake kuwa washindani wakuu ligini muhula huu.

Hata hivyo, kwa sasa Atletico wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 77 huku pengo la pointi mbili pekee likitamalaki kati yao na nambari mbili Barcelona. Real ya kocha Zinedine Zidane inakamata nafasi ya tatu kwa alama 74, nne zaidi kuliko Sevilla.

Mchuano kati ya Real na Barcelona ulimpa Suarez, 34, fursa ya kurejea Camp Nou kupepetana na waajiri wake wa zamani. Alimkumbatia sana rafiki yake Messi mwanzoni mwa mchezo na hata baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kimya cha Kiunjuri kuhusu 2022 chazua gumzo

Real, Barcelona na Juventus watetea kuhusika kwao kwenye...