• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kimya cha Kiunjuri kuhusu 2022 chazua gumzo

Kimya cha Kiunjuri kuhusu 2022 chazua gumzo

Na JAMES MURIMI

KIONGOZI wa chama cha The Service Party (TSP), Bw Mwangi Kiunjuri, amebaki kimya kuhusu mipango yake ya kisiasa huku uchaguzi mkuu ujao unapoendelea kukaribia.

Bw Kiunjuri amewaacha Wakenya wengi wakiuliza maswali kuhusu ikiwa atawania ubunge katika eneo la Laikipia Mashariki au ugavana katika Kaunti ya Laikipia.

Bw Kiunjuri, aliyehudumu pia kama Waziri wa Kilimo, pia anadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya viongozi katika eneo la Mlima Kenya kuwa mgombea-mwenza wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kwenye uchaguzi huo.

Duru ziliiambia Taifa Jumapili kwamba mwanasiasa huyo bado hajaamua ikiwa atawania nafasi yoyote ya kisiasa.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni majuzi, Bw Kiunjuri alikanusha madai kuwa ameahidiwa nafasi ya kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto.

“Ikiwa nimeahidiwa nafasi hiyo na rafiki yangu Dkt Ruto, basi nisingebuni TSP. Badala yake ningejiunga na chama cha UDA na kungoja kuungwa mkono,” akasema.

Alisema Dkt Ruto ana uhuru wa kushauriana na viongozi na wenyeji wa Kati kuhusu chaguo la atayakekuwa mgombea-mwenza wake.

“Mnamo 2013, Rais Kenyatta alikuwa katika chama cha TNA wakati Dkt Ruto akiwa katika URP. URP haikumzuia Dkt Ruto kuwa mgombea-mwenza wa Rais katika uchaguzi huo. Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa Bw Raila Odinga na Bw Kalonzo Musyoka, walio katika vyama vya ODM na Wiper mtawalia,” akasema Bw Kiunjuri.

Alisema ametosheka kwenye nafasi yake kama kiongozi wa TSP lakini akaeleza, “Alichokibariki Mungu, hakuna mwanadamu anayeweza (ku)kilaani.”

Alisema anamheshimu Rais Kenyatta na hajawahi kuukosoa ama kuudharau uongozi wake.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI: Yaelekea huu ndio mwanzo mpya EAC

Barcelona na Atletico Madrid nguvu sawa katika Ligi Kuu ya...