• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Barcelona wacharaza Eibar na kukamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya tatu jedwalini

Barcelona wacharaza Eibar na kukamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya tatu jedwalini

Na MASHIRIKA

ANTOINE Griezmann alifunga bao katika dakika ya 81 na kusaidia waajiri wake Barcelona kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu katika nafasi ya tatu jedwalini.

Ni mara ya kwanza kwa mabingwa hao mara 26 wa La Liga kukamilisha kampeni za kivumbi hicho nje ya mduara wa mbili-bora tangu 2007-08.

Goli la Griezmann ambaye ni raia wa Ufaransa lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi Ousmane Dembele ambaye pia ni raia wa Ufaransa.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walifanyika kikosi chao mabadiliko makubwa katika mchuano huo uliowashuhudia wakicheza bila huduma za wanasoka wengi tegemeo akiwemo Lionel Messi aliyepewa likizo ya mapema ili kujiandaa kwa fainali za Copa America zitakazoandaliwa na taifa lake la Argentina kati ya Juni 13 na Julai 11, 2021.

Barcelona kwa sasa wanakamilisha kampeni huu wa 2020-21 kwenye La Liga wakiwa wamejizolea alama 79, saba zaidi nyuma ya Atletico Madrid waliotawazwa wafalme kwa mara ya kwanza tangu 2013-14 baada ya kuwapepeta Real Valladolid 2-1 mnamo Mei 22, 2021.

“Hatukujituma jinsi ilivyohitajika katika mechi muhimu msimu huu. Ninafurahia bao nililofunga dhidi ya Eibar japo ninasikitishwa na jinsi ambavyo msimu huu umetamatika bila ya Barcelona kujizolea taji. Hatukuanza vyema kampeni zetu za muhula huu. Tulifufua makali yetu mwanzoni mwa mwaka wa 2021,” akasema Griezmann aliyejiunga na Barcelona mnamo 2019 baada ya kuagana na Atletico.

“Nawapongeza Atletico kwa ufanisi wao. Namhongera kocha Diego Simeone, marafiki zangu wote na mashabiki wa wafalme wapya wa La Liga. Atletico kwa kweli walistahili ubingwa wa muhula huu,” akaongeza Griezmann.

Mbali na Messi, wanasoka wengine waliokosa kuunga kikosi cha Barcelona dhidi ya Eibar ni Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Clement Lenglet, Jordi Alba na Pedri Lopez.

Eibar waliingia katika mchuano huo wakiwa tayari wameshuka ngazi kutoka La Liga baada ya kujizolea jumla ya alama 30 pekee msimu huu. Wanateremka daraja kwenye La Liga kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka saba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kisumu ingali juu kwa visa vipya vya corona

Idadi ya vijana kwenye kilimo na ufugaji ni ya chini mno...