• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Barcelona waponda Real Madrid katika gozi la El Clasico

Barcelona waponda Real Madrid katika gozi la El Clasico

Na MASHIRIKA

KOCHA Xavi Hernandez amesema waajiri wake Barcelona wana uwezo wa kujizolea taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu baada ya kuponda Real Madrid 4-0 katika gozi la El Clasico mnamo Jumapili usiku ugani Santiago Bernabeu.

Real waliojibwaga ugani wakiwinda ushindi wa sita mfululizo katika El Clasico wangali wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 66, tisa zaidi kuliko nambari mbili Sevilla ambao pia wametandaza mechi 29 sawa na Real.

Barcelona wanakamata nafasi ya tatu kwa pointi 54 sawa na mabingwa watetezi Atletico Madrid wanaofunga orodha ya nne-bora. Hata hivyo, nafuu zaidi kwa Barcelona ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi 29 ambayo imetandazwa na washindani wao wakuu – Real, Sevilla na Atletico.

Fowadi wa zamani wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang alifungia Barcelona mabao mawili na kuchangia jingine lililojazwa kimiani na Ferran Torres katika gozi hilo la El Clasico.

Aubameyang na Ronald Araujo walifunga mabao yao kutokana na krosi za Ousmane Dembele katika kipindi cha kwanza. Torres alifungia Barcelona bao la tatu katika dakika ya 47 kabla ya Aubayemang kuzamisha kabisa chombo cha Real kunako dakika ya 51.

Chini ya kocha Xavi, Barcelona kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kutokana na 12 zilizopita.

“Sijui kama tutashinda taji la La Liga. Hakuna kisichowezekana. Pengine tulichelewa kidogo kuanza kufukuzia taji hili, lakini ushindi huu dhidi ya Real unastahili kutuaminisha hata zaidi,” akasema Xavi.

“Tulicheza vizuri zaidi kuliko Real. Tulicheza kama kikosi kilichokuwa nyumbani. Ilikuwa raha kwangu, kwa wachezaji, usimamizi na mashabiki wetu. Tungalifunga mabao zaidi katika mchuano huo ambao naamini utakuwa mwanzo wa kubadilika kwa matokeo yajayo ya mechi za El Clasico,” akaongeza.

“Tungali na fursa ya kutwaa ubingwa wa La Liga. Tutapigania taji hili hadi mwisho. Huenda nafasi hiyo kwa sasa ikaonekana kuwa finyu lakini chochote kinawezekana katika soka. Sisi ni Barcelona,” akasema kiungo wa Barcelona, Sergio Busquets.

Kocha wa Real, Carlo Ancelotti alisema ndiye aliyestahili kulaumiwa kwa kichapo kinono ambacho kikosi chake kilipokezwa. Hata hivyo, aliwataka masogora wake kujinyanyua upesi na kumakinikia michuano ijayo.

Barcelona wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya Xavi aliyejaza nafasi ya kocha Ronald Koeman mnamo Novemba 2021. Tangu wakati huo, wamepoteza mara moja pekee katika La Liga na hiyo ilikuwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita.

Ufufuo huo umechangiwa zaidi na sajili wapya waliotokea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) – Aubameyang kutoka Arsenal, Torres kutoka Man-City na Adama Traore aliyetokea Wolves.

Hadi kufikia sasa, ni Memphis Depay pekee (mabao 10) ambaye amefungia Barcelona magoli mengi zaidi msimu huu kuliko Aubameyang (tisa) na Torres (matano).

Japo matumaini ya kunyanyua taji la La Liga ni finyu, matokeo dhidi ya Real ni ishara ya kurejea kwa uthabiti wa Barcelona ambao sasa wanatazamiwa kuwa mwiba mkali kwa washindani wao wakuu katika La Liga na soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Ushindi dhidi ya Real ulikuwa wao wa kwanza katika kipindi cha miaka mitatu na mnono zaidi ugani Bernabeu tangu 2015. Real walikosa huduma za fowadi Karim Benzema aliyewasaidia kudengua Paris Saint-Germain (PSG) katika hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 9, 2022. Kufikia sasa, Benzema ambaye ni raia wa Ufaransa, amefungia Real mabao 22 na kuchangia 11 mengine msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Elisha Otoyi

Boga aomba ODM tiketi bila mchujo

T L