• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Boga aomba ODM tiketi bila mchujo

Boga aomba ODM tiketi bila mchujo

NA SIAGO CECE

ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga, ameomba Chama cha ODM kimpe tiketi ya moja kwa moja kuwania ugavana Kwale katika uchaguzi ujao.

Mchuano wa tiketi hiyo umevutia wanasiasa wengine akiwemo Seneta Maalumu, Dkt Agnes Zani, Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale, Bw Sammy Ruwa, na aliyekuwa mhandisi wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA), Bw Chai Lung’anzi.

Prof Boga alisema ijapokuwa amejiandaa vilivyo kwa kura ya mchujo dhidi ya wapinzani wake, ODM ingelizingatia kumpa tiketi ya moja kwa moja kwa vile anaamini yeye ndiye mgombeaji maarufu.

“Tayari tunaongoza na tumehakikisha kuwa chama kimepata umaarufu Kwale. Tumeshawasilisha ombi letu kwa chama na tuna uhakika kwamba ili kusiwe na vita nikuvute, chama kitatoa uamuzi ambao utawafurahisha wakazi wa Kwale,” akasema.

Wanasiasa hao wanaendelea na kampeni zao wakilenga kuongeza idadi ya wafuasi wao na umaarufu.Licha ya hayo, katibu huyo aliyejiuzulu ili kujitosa kwa siasa alisema kuwa tayari ameweka hatua ya kuhakikisha kuwa endapo kutakuwa na kura ya mchujo, utafanywa kwa njia ya haki ili kuepusha malumbano yoyote.

Wakati huo huo, alimrushia ndoano Bw Lung’anzi akitaka kumshawishi kuungana naye kabla ya kura za uteuzi mwezi ujao.

Prof Boga alisema hayo mwishoni mwa juma alipokuwa akiwapokea baadhi ya wanachama wa waliokuwa wakiegemea upande wa Bw Lung’anzi ambao waliamua kujiunga na kikosi chake.

“Ikiwa Lung’anzi yuko tayari kufanya kazi nasi, basi namkaribisha kuniunga mkono. Hii ndiyo sababu ya sisi kuwa hapa,” Prof Boga alisema.

Hapo awali Bw Lung’anzi alikuwa amesema kuwa watashiriki na Bw Boga katika mchujo, na atakayeshinda atamuunga mkono mwenzake.

Haya yanajiri huku akiimarisha kampeni za muungano wa Azimio la Umoja katika kaunti ya Kwale, ili kumpigia debe kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kwa urais katika uchaguzi ujao.

Prof Boga alisema Bw Odinga anatarajiwa kuandaa mikutano zaidi katika kaunti hiyo miezi ijayo.

Kulingana naye, ODM bado ni maarufu katika kaunti hiyo hata kama haikufanikiwa kushinda kiti cha ugavana katika uchaguzi uliopita.

“Ndiyo, Gavana Salim Mvurya alihamia Jubilee, lakini hakushinda kwa sababu ya chama, bali kwa sababu ya umaarufu wake. Lakini viongozi wengine wote wa kaunti wako katika ODM akiwemo spika na kiongozi wa wengi katika bunge. Hii ndiyo maana sisi ni ngome ya ODM,” akasema.

Alipuuzilia mbali madai ya wakosoaji kwamba Kwale imekuwa ngome ya Kenya Kwanza baada ya wabunge wote kujiunga na vuguvugu hilo.

Alidai kuwa wabunge waliojiunga na Kenya Kwanza na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) walifanya hivyo kwa sababu zao za kibinafsi wala sio kwa kujali maslahi ya Kaunti ya Kwale.

Wanasiasa wengine wanaotaka kurithi kiti cha Bw Mvurya katika kaunti hiyo ni Naibu Gavana, Bi Fatuma Achani (UDA), aliyekuwa Mbunge wa Matuga, Bw Chirau Ali Mwakwere (Wiper) na mfanyabiashara Gereza Dena (KANU).

You can share this post!

Barcelona waponda Real Madrid katika gozi la El Clasico

Liverpool wapewa Man-City, Palace wakivaana na Chelsea...

T L