• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Barnaba Korir: Tuko tayari kuandaa Kip Keino Classic

Barnaba Korir: Tuko tayari kuandaa Kip Keino Classic

AYUMBA AYODI na IAAF

KENYA iko tayari kuandaa tena duru ya mashindano ya riadha ya Continental Tour Gold ya Kip Keino Classic itakayokuwa ya mwisho kwenye orodha ya duru 12.

Imeratibiwa kufanyika Septemba 18 ugani Nyayo.

Msimu utang’oa nanga Aprili 24 na duru ya USATF Grand Prix katika uwanja wa Hayward Field mjini Oregon utakaoandaa Riadha za Dunia mwaka 2022.

Litakuwa shindano la kwanza uwanjani Hayward Field tangu ukarabatiwe kwa hivyo utawapa washiriki kionjo cha mashindano ya dunia yatakavyokuwa.

Baada ya shindano hilo katika Chuo Kikuu cha Oregon, wanariadha wataelekea nchini Japan kwa duru ya pili inayoitwa ‘Ready Steady Tokyo’ mnamo Mei 9. Itakuwa majaribio ya michezo ya Olimpiki mjini Tokyo.

Duru hii itafanyika majuma mawili 12 tu kabla ya Olimpiki kuanza. Itawapa wanariadha fursa ya kutumia vifaa vya kisasa vitakavyotumiwa na timu zitakazoshiriki Olimpiki mnamo Julai 23 hadi Agosti 8. Eneo hilo litatumiwa kwa hafla ya kufungua na kufunga michezo ya Olimpiki.

Duru ya tatu (USATF Golden Games) itafanyika siku hiyo mjini California.

Siku 10 baadaye, wanariadha wataelekea barani Ulaya kwa makala ya 60 ya Golden Spike mjini Ostrava nchini Czech mnamo Mei 19 na kurejea Amerika mnamo Mei 23 kwa duru ya Adidas Boost Boston Games.

Msimu uliopita, duru sita kati ya 12 ikiwemo Kip Keino Classic, zilifanyika licha ya changamoto zinazotokana na janga la virusi vya corona.

Mabingwa wa dunia Hellen Obiri (mbio za mita 5,000) na mshikilizi wa rekodi ya dunia Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) ni baadhi ya Wakenya waliong’ara katika shindano la Kip Keino Classic.

“Kwa mara nyingine tena tuko tayari na tuna hamu kubwa ya kuandaa shindano nzuri. Tunatumai kuvutia wanariadha nyota na pia kuwa na mashabiki uwanjani,” alisema mkurugenzi wa mbio za Kip Keino, Barnaba Korir.

Kalenda ya Continental Tour Gold (2021):

Aprili 24 – USATF Grand Prix, Eugene (Amerika)

Mei 9 – Ready Steady Tokyo, Tokyo (Japan)

Mei 9 – USATF Golden Games, Walnut (Amerika)

Mei 19 – Golden Spike, Ostrava (Czech)

Mei 23 – Adidas Boost Boston Games, Boston (Amerika)

Juni 6 – FBK Games, Hengelo (Uholanzi)

Juni 8 – Paavo Nurmi Games, Turku (Finland)

Jun 30 – Irena Szewinska Memorial, Bydgoszcz (Poland)

Julai 6 – Gyulai Memorial, Szekesfehervar (Hungary)

Septemba 5 – Skolimowska Memorial, Silesia (Poland)

Septemba 14 – Hanzekovic Memorial, Zagreb (Croatia)

Septemba 18 – Kip Keino Classic, Nairobi

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Inter Milan sasa pua na mdomo kutwaa taji la Serie A kwa...

Keki anazooka zinapendwa na wateja kote nchini