• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Blatter, Platini waponea kifungo kwa kuondolewa madai ya ulaghai

Blatter, Platini waponea kifungo kwa kuondolewa madai ya ulaghai

NA MASHIRIKA

BELLINZONA, Uswisi

SEPP Blatter na Michel Platini wamepatikana na mahakama nchini Uswisi bila hatia ya ulaghai baada ya majuma mawili ya kusikilizwa kwa kesi kuhusu malipo ya Sh225.6 milioni yaliyofanywa 2011.

Marais hao wa zamani wa mashirikisho ya soka duniani (FIFA) na Ulaya (UEFA) mtawalia walifahamu mapema jana hatima yao katika hukumu iliyotangazwa na majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo mwezi Juni.

Licha ya kuondolewa mashtaka hayo, Blatter, 86, ataendelea kutumikia marufuku dhidi ya kujihusisha na soka hadi 2028 kwa adhabu nyingine tofauti mwaka 2021. Platini, 67, amekamilisha marufuku yake. Wote walipigwa marufuku 2015. Wangepatikana na hatia huenda wangefungwa jela hadi miaka mitano ama kutozwa faini.

Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG) ilikuwa imeshtaki Blatter na Platini kwa “ulaghai, matumizi mabaya, usimamizi mbaya pamoja na kughushi stakabadhi.”

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Blatter alitaja fedha Sh225.6 milioni zilizotumiwa Platini kama “makubaliano ya kirafiki” kwa kazi ambayo kiungo huyo wa zamani wa Ufaransa alikuwa amefanya ya kushauri Blatter kati ya 1998 na 2002.

Platini alitaka alipwe Sh115.2 milioni (pauni 816,000) kila mwaka, lakini Blatter alisema kuwa shirikisho hilo halina uwezo wa kumlipa mshahara huo.

Badala yake, mshindi huyo wa mataji matatu ya mwanasoka bora duniani (Ballon d’Or) alisaini kandarasi kupokea Sh36.2 milioni kila mwaka, na kwa mujibu wa Blatter, walikuwa wameelewana kupitia kinywa tu kuwa fedha zilizosalia atalipwa baadaye.

Majukumu hayo ya kutoa ushauri yalikatika 2002. Hakuna malipo zaidi yalitajwa katika kandarasi iliyotiwa saini.

  • Tags

You can share this post!

Maadhimisho ya Idd yaanza leo Jumamosi wauzaji mifugo...

DOUGLAS MUTUA: Uhuru wa kutungua mimba kiholela haufai

T L