• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Brighton wapoteza penalti mbili nalo bao lao la utata dhidi ya West Brom likifutiliwa mbali na VAR

Brighton wapoteza penalti mbili nalo bao lao la utata dhidi ya West Brom likifutiliwa mbali na VAR

Na MASHIRIKA

BRIGHTON walipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa wenyeji West Bromwich Albion katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia wageni wakipoteza nafasi nyingi za wazi.

Refa Lee Mason alikataa kuhesabu bao la Brighton baada ya kurejelea VAR huku kikosi hicho cha kocha Graham Potter kikipoteza pia mikwaju miwili ya penalti.

Bao kutokana na frikiki iliyochanjwa na Lewis Dunk wa Brighton katika kipindi cha kwanza lilikataliwa mwanzo, kabla ya kukubaliwa kisha kufutiliwa mbali kabisa na Mason aliyechukua muda mrefu kurejelea VAR.

Beki wa Brighton Lewis Dunk (kulia) azungumza na refarii Lee Mason wakati wa mapumziko wenyeji West Bromwich Albion walipokaribisha Brighton and Hove Albion katika uwanja wa The Hawthorns, Februari 27, 2021. Picha/ AFP

Beki Kyle Bartley aliwafungia West Brom bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo kunako dakika ya 11. Japo Brighton walipania kurejea mchezoni, walishuhudia kombora la Pascal Gross likibusu mwamba wa goli kabla ya Danny Welbeck kupoteza penalti ya kwanza.

Wanasoka wengine wa Brighton waliopoteza nafasi tele za wazi katika mechi hiyo iliyoshuhudia wageni wakimiliki asilimia kubwa ya mpira na kudhibiti mchuano mzima ni Neal Maupay na Aaron Connolly.

Matokeo hayo yaliwasaza West Brom wanaotiwa makali na kocha Sam Allardyce katika nafasi ya 19 kwa alama 17, tisa nyuma ya Newcastle walioko nje ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho.

Ushindi uliosajiliwa na West Brom ulikuwa wao wa kwanza katika uwanja wa nyumbani chini ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Brighton waliingia ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakitarajiwa kusajili ushindi baada ya chombo chao kuzamishwa tena na Crystal Palace katika mchuano wa awali ligini.

West Brom kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Everton uwanjani Hawthorns mnamo Alhamisi ya Machi 4 huku Brighton wakiwaalika Leicester City mnamo Machi 6 ugani Amex.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Leicester City kurefusha mkataba wa fowadi Harvey Barnes...

Jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa biriani ya nyama ya mbuzi