• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:32 PM
Brighton yadhalilisha Man-United katika pambano la EPL uwanjani Amex

Brighton yadhalilisha Man-United katika pambano la EPL uwanjani Amex

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walidhalilishwa na Brighton kwa kichapo cha 4-0 ugani Amex katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza ambayo matokeo yake yalithibitisha kwamba mabingwa hao mara 20 wa EPL hawatafuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2022-23.

Nyota raia wa Ecuador, Moises Caicedo, aliwaweka wenyeji Brighton kifua mbele kunako dakika ya 15. Bao hilo lilikuwa lake la kwanza ligini katika mechi ya sita ndani ya jezi za Brighton. Goli hilo lilichangiwa na utepetevu wa beki wa Man-United, Alex Telles, aliyeshindwa kuondoa mpira katika eneo la hatari.

Kocha mshikilizi wa Man-United, Ralf Rangnick sasa amesalia na mchuano mmoja pekee wa kusimamia kambini mwa Man-United – dhidi ya Crystal Palace mnamo Mei 22, 2022 ugani Selhurst Park – kabla kumpisha mkufunzi mpya, Erik ten Hag anayetarajiwa kuagana na Ajax ya Uholanzi.

Marc Cucurella alifunga bao la pili la Brighton baada ya kukamilisha krosi ya Leandro Trossard katika dakika ya 49 kabla ya Pascal Gross kujaza kimiani goli la tatu kunako dakika ya 57. Trossard alizamisha kabisa chombo cha Man-United katika dakika ya 60.

Mechi hiyo ilikuwa ya tano mfululizo kwa Man-United kupoteza ugenini na matokeo hayo yanamaanisha kwamba hawawezi sasa kukamilisha kampeni za EPL msimu huu juu ya nafasi ya sita. Ni vikosi vinne pekee kutoka EPL vitakavyofuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao.

Itakuwa mara ya tano katika kipindi cha miaka 30 kwa Man-United kutonogesha soka ya bara Ulaya na sasa wako katika hatari ya kukosa kipute cha Europa League na hivyo kushuka kwa ligi ndogo zaidi ya Europa Conference League iwapo watashindwa kuhimili ushindani mkali kutoka kwa West Ham United na Wolves.

Kufikia sasa, Man-United wanakamata nafasi ya sita kwa alama 58, sita zaidi kuliko West Ham ambao wana mechi mbili zaidi za akiba ili kufikia idadi ya michuano 37 ambayo tayari imesakatwa na masogora hao wa Rangnick.

Mechi hiyo iliyokutanisha Brighton na Man-United ilihudhuriwa na mashabiki 31,637, hicho kikiwa kiasi kikubwa zaidi cha mahudhurio ya mashabiki ugani Amex.

Ni ushindi uliodhihirisha pia ukubwa wa kiwango cha uthabiti wa Brighton ambao waliambulia sare dhidi ya Liverpool msimu huu, kupokonya Arsenal alama nne, kupepeta Tottenham Hotspur ugenini na kulazimishia Chelsea sare nyumbani na ugenini.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Brighton kushinda mechi katika uwanja wao wa nyumbani mwaka huu wa 2022 baada ya kujizolea alama nne pekee kutokana na michuano minane iliyopita ugani Amex.

Isitoshe, ufanisi huo dhidi ya Man-United uliweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya orodha ya 10-bora kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 121.

Kwa Man-United, wanachotazamia sasa ni kampeni za msimu huu kutamatika rasmi ikizingatiwa kwamba hawajafikia mengi ya matarajio yao hasa baada ya kumwaga sokoni kima cha Sh18.7 bilioni mwanzoni mwa muhula huu kwa ajili ya huduma za Raphael Varane, Jadon Sancho na mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo.

Yalikuwa matarajio ya mashabiki wa Man-United kwamba kikosi hicho kingejizolea taji la EPL msimu huu hasa baada ya kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Manchester City mnamo 2020-21.

Hata hivyo, kocha Ole Gunnar Solskjaer alipigwa kalamu mnamo Novemba 2021 na nafasi yake kutwaliwa na Rangnick aliyenyimwa fursa ya kusajili wachezaji wapya zaidi mnamo Januari 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanawake 3 wafungwa jela miezi sita kwa kuiba simu ya...

Spurs walazimishia Liverpool sare katika EPL ugani Anfield

T L