• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Spurs walazimishia Liverpool sare katika EPL ugani Anfield

Spurs walazimishia Liverpool sare katika EPL ugani Anfield

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walipoteza alama mbili muhimu kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Anfield tangu Oktoba 2021 baada ya Tottenham Hotspur kuwalazimishia sare ya 1-1 mnamo Jumamosi usiku.

Matokeo hayo yaliwapaisha Liverpool kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 83 kwa wingi wa mabao. Hata hivyo, Manchester City watawapiku mnamo Mei 8, 2022 iwapo watatandika Newcastle United uwanjani Etihad. Man-City ambao wana mechi moja zaidi ya akiba ili kufikia idadi ya michuano 35 ambayo imetandazwa na Liverpool, wanakamata nafasi ya pili jedwalini kwa alama 83.

Son Heung-min aliwaweka Spurs kifua mbele katika dakika ya 56 baada ya kushirikiana na Harry Kane na Ryan Sessegnon kabla ya Luis Diaz kusawazishia Liverpool kunako dakika ya 74.

Ingawa bao hilo liliamsha motisha ya Liverpool, Spurs walibana sana ngome yao na kusambaratisha mipango yote ya mafowadi wa Liverpool.

“Sioni sasa Man-City wakipoteza alama zaidi. Sare hii dhidi ya Spurs itawapa motisha zaidi na wapo pazuri kuhifadhi taji la EPL msimu huu,” akasema kocha Jurgen Klopp wa Liverpool.

Licha ya sare, Liverpool waliendeleza rekodi yao ya kutopigwa katika EPL katika mechi 16, ikiwemo mechi 13 mfululizo huku wakiambulia sare mara tatu. Spurs kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 62, moja nyuma ya Arsenal wanaofunga orodha ya nne-bora.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Brighton yadhalilisha Man-United katika pambano la EPL...

Ukarimu wa Ruto wampa makanisa

T L