• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Bruno Fernandes asema hataachia Ronaldo jukumu la kuchanja penalti za Man-United

Bruno Fernandes asema hataachia Ronaldo jukumu la kuchanja penalti za Man-United

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Manchester United, Bruno Fernandes, amesema ataendelea kuchanja penalti za waajiri wake japo kwa “ukakamavu zaidi bila kuhofia lolote” baada ya kupoteza mkwaju wa Jumamosi dhidi ya Aston Villa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota huyo raia wa Ureno alipaisha penalti ya dakika za mwisho ambayo vinginevyo ingaliwapa Man-United alama moja muhimu katika mechi hiyo iliyoshuhudia Villa wakisajili ushindi wa 1-0 uliokuwa wao wa kwanza katika kipindi cha miaka 12 dhidi ya mabingwa hao mara 20 wa EPL ugani Old Trafford.

“Kwa mara nyingine, nilikubali jukumu nililopewa na waajiri wangu. Ingawa nilizamisha matarajio ya mashabiki, niko tayari kuendelea kutekeleza jukumu hilo bila hofu yoyote iwapo nitaaminiwa fursa nyingine ya kufanya hivyo,” akasema Fernandes.

“Asanteni kwa kunitilia shime baada ya mechi dhidi ya Villa. Kusikia jinsi mlivyoimba jina langu uwanjani ni jambo lililonipa ujasiri zaidi. Nitarejea kwa matao ya juu zaidi kwa sababu nafahamu ni wajibu wangu kudumisha viwango bora,” akaongeza sogora huyo wa zamani wa Sporting CP ya Ureno.

Baada ya kupoteza penalti hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa Man-United kupokezwa ligini muhula huu, kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kiliteremka hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 13 sawa na Everton, Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City.

Ushindi kwa Man-United ungaliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali kwa pointi 16 baada ya Chelsea kulazwa na Man-City nao Liverpool kulazimishiwa sare ya 3-3 na limbukeni Brentford. Chini ya mkufunzi Jurgen Klopp, viongozi Liverpool (alama 14) ndiyo klabu ya pekee kufikia sasa ambayo haijapoteza mechi yoyote kati ya sita zilizopita ligini.

Baada ya supastaa Cristiano Ronaldo kuagana na Juventus ya Italia na kurejea ugani Old Trafford msimu huu, mjadala kuhusu nani kati ya Fernandes na nyota huyo wa zamani wa Real Madrid angekuwa akipiga penalti za Man-United uliibuka.

Licha ya kupoteza penalti iliyopita dhidi ya Villa, Fernandes angali anajivunia rekodi nzuri ya kuchanja matuta katika soka ya ngazi ya klabu. Ana asilimia 90.7 ya ufanisi baada ya kufunga mikwaju 39 kati ya 43 iliyopita. Ronaldo ambaye pia ni mwenzake katika timu ya taifa, anajivunia asilimia 85 ya mafanikio baada ya kupachika wavuni penalti 125 kutokana na 147.

Kwingineko, kocha Pep Guardiola wa Man-City amekiri kwamba kichapo ambacho masogora wake walipokeza Chelsea katika mchuano uliopita ligini ni ishara ya kiu yao ya kutaka kuhifadhi ufalme wa kipute hicho muhula huu.

Mbali na ushindi huo kumfanya Guardiola kuwa mkufunzi ambaye sasa anajivunia ufanisi mkubwa zaidi katika historia ya waajiri wake kwa kushinda mechi 221 kutokana na mashindano yote, Man-City walisalia miongoni mwa wawaniaji halisi wa ubingwa wa EPL msimu huu.

“Tunashikilia nafasi nzuri jedwalini na matokeo yetu ni ya kuridhisha licha ya Man-City kukosa huduma za mshambuliaji mkuu ambaye ni tegemeo la kikosi,” akatanguliza mkufunzi huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

“Mara nyingine nalazimika kuamini kwamba tunahitaji fowadi wa kumalizia krosi za viungo wetu. Hata hivyo, kikosi kingali thabiti sawa na msimu jana ambapo tulitawazwa wafalme licha ya mvamizi mkuu Sergio Aguero kusalia mkekani kwa kipindi kirefu cha kampeni za muhula huo,” akaongeza.

Guardiola kwa sasa anatazamia kuongoza Man-City kupepetana na Paris Saint-Germain (PSG) katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 28, 2021 kabla ya kushuka ugani Anfield kupimana ubabe na Liverpool ligini wikendi hii.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI: Nyota ya kisiasa ya Karua inaingia doa?

Juventus waingia ndani ya 10-bora jedwalini baada ya...