• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
CAF: Kipi kitarajiwe mechi ya Gor Mahia dhidi ya CR Belouizdad?

CAF: Kipi kitarajiwe mechi ya Gor Mahia dhidi ya CR Belouizdad?

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Algeria, CR Belouizdad waliwasili humu nchini mnamo Januari 3 kwa mchuano wa mkondo wa pili wa Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Gor Mahia.

Mechi hiyo ya marudiano inasakatwa leo Jumatano katika uwanja wa Nyayo kuanzia saa tisa alasiri.

Gor Mahia watahitaji kufunga Belouizdad angalau mabao saba bila jibu ili kufuzu kwa hatua ya makundi. Hii ni baada ya miamba hao wa humu nchini kupokezwa kichapo cha 6-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Algiers mnamo Disemba 26, 2020.

Kichapo ambacho Gor Mahia walipokezwa na Belouizdad kilihusishwa na mikakati duni na maandalizi mabovu yaliyoshuhudia kikosi hicho kilichoongozwa na kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo kikiwasili Algiers siku moja kabla ya mechi.

Gor Mahia walikabiliwa na panda-shuka tele za usafiri baada ya kulazimika kupitia jijini Doha, Qatar kabla ya kuelekea Algiers.

Kabla ya kuondoka humu nchini kwa minajili ya mechi hiyo iliyopangiwa awali kusakatwa Disemba 23 kabla ya Gor Mahia kuomba Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) iratibu upya, wanasoka wa K’Ogalo walikuwa wamesusia mazoezi wakilalamikia kutolipwa malimbikizi ya mishahara na marupurupu.

Hali si tofauti na hata sasa ambapo wachezaji wa kikosi hicho wamekuwa wakigomea mazoezi kwa madai ya kutolipwa mishahara na marupurupu yao.

Kwa mujibu wa mhazini wa Gor Mahia, Dolphin Odhiambo, suala hilo limezima kabisa matumaini ya kikosi japo amelaumu ulimbukeni wa kocha Omollo katika ulingo wa soka ya kimataifa kwa kichapo kinono walichopokezwa nchini Algeria.

“Yalikuwa matokeo ya aibu kusajiliwa na kikosi kikubwa kufu ya Gor Mahia. CAF ni kivumbi chenye ushindani mkali na washiriki huhitaji maandalizi ya kutosha kwa wakati ufaao na kikosi huhitaji pia kocha mwenye tajriba pevu na uzoefu mpana,” akasema Odhiambo.

Kiungo Amir Sayoud, 30, alifungia Belouizdad mabao matatu kabla ya mengine kufumwa wavuni na Hamza Bellahouel, Larbi Tabti na Maecky Ngombo katika mechi hiyo iliyochezewa ugani 1955 Stadium.

Baadhi ya wanasoka wa Gor Mahia walitarajiwa kushiriki mazoezi uwanjani Nyayo mnamo Januari 5 kabla ya kuwapisha wapinzani wao Belouizdad kuandaa kipindi kimoja cha mazoezi ugani humo alasiri.

Kwa mujibu wa CAF, Mechi ya marudiano kati ya Gor Mahia na Belouizdad itasimamiwa na refa Bernard Hensel Camille kutoka Ushelisheli akisaidiwa na Hensley Danny Petrousse, Steve Marie na Eldrick Matthieu Adelaide ambao pia ni raia wa Ushelisheli.

Zam Ali kutoka Zanzibar atakuwa kamishna wa mechi huku daktari wa Tusker FC, Wycliffe Makanga akiteuliwa kuwa afisa wa kushughulikia matukio yoyote yatakayohusiana na visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

WANGARI: Serikali ibuni mbinu kabambe za kukusanya kodi...

TAHARIRI: Serikali ilipaswa kuboresha shule