• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Cavani kuendelea kusakatia Man United hata baada ya msimu huu

Cavani kuendelea kusakatia Man United hata baada ya msimu huu

CHRIS ADUNGO Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer amefichua kwamba Manchester United wana mpango wa kurefusha mkataba wa fowadi Edinson Cavani baada ya kandarasi yake ya sasa uwanjani Old Trafford kutamatika mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

“Cavani angali na miaka michache ya kusakata soka ya ushindani mkubwa. Sioni chochote kitakachozuia usimamizi wa Man-United kurefusha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwetu. Ninamwamini sana na tayari amedhihirisha ukubwa wa uwezo alio nao katika kufanya mambo makuu katika idara ya mbele,” akatanguliza mkufunzi huyo raia wa Norway.

“Cavani si sogora wa kupangwa mechini akitokea benchi. Ataanza kupangwa katika kikosi cha kwanza hivi karibuni. Ushawishi aliojivunia PSG na Napoli ungalipo na atakuwa miongoni mwa wavamizi tegemeo wa Man-United kwa mihula michache ijayo,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Norway.

“Anafahamu matarajio ya mashabiki kutoka kwake ikizingatiwa kwamba anavalia jezi nambari saba iliyowahi kuvaliwa na wanasoka nguli wa Man-United wakiwemo Antonio Valencia, George Best, Bryan Robson, David Beckham na Cristiano Ronaldo,” akasisitiza Solskjaer.

Tangu atie guu ugani Old Trafford baada ya kubanduka Paris Saint-Germain (PSG), Cavani, 33, amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Man-United mara mbili pekee kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mara ya mwisho zaidi ikiwa katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Wolves mnamo Disemba 29, 2020 ugani Old Trafford.

Hata hivyo, amefunga mabao matatu kutokana na michuano minane huku akitokea benchi na kuchangia goli lililojazwa wavuni na Bruno Fernandes dhidi ya Leicester City mnamo Disemba 26, 2020.

Ujio wa Cavani ugani Old Trafford umechangia kuimarika kwa makali ya safu ya mbele ya Man-United ambayo imekuwa ikiongozwa na washambuliaji chipukizi Marcus Rashford, Anthony Martial na Mason Greenwood.

Hadi kuingia kwake Man-United, Cavani alikuwa amefunga jumla ya mabao 341 kutokana na mechi 556 alizocheza katika kiwango cha klabu. Mabao 200 kati ya hayo yalitokana na mechi 301 alizopigia PSG ambao ni miamba wa soka ya Ufaransa. Cavani anajivunia pia kufungia timu ya taifa ya Uruguay jumla ya mabao 51 kutokana na mechi 117.

Ingawa PSG walikuwa radhi kurefusha mkataba wa Cavani ugani Parc des Princes, kuondoka kwake kambini mwa wanafainali hao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 kulichochewa na mizozo ya mara kwa mara kati yake na mfumaji raia wa Brazil, Neymar Jr.

You can share this post!

Olunga kulenga juu zaidi baada ya makali yake ugani...

IEBC yaomba radhi kwa kuita BBI ‘Burning Bridges...