• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Chelsea kuuza wanasoka saba mwezi huu wa Januari 2021 kwa lengo la kujinasia huduma za Erling Haaland na Declan Rice

Chelsea kuuza wanasoka saba mwezi huu wa Januari 2021 kwa lengo la kujinasia huduma za Erling Haaland na Declan Rice

Na MASHIRIKA

MIPANGO ya Chelsea katika muhula mfupi ujao wa uhamisho wa wachezaji imefichuka huku mabadiliko makubwa yakitarajiwa.

Kikosi hicho cha kocha Frank Lampard kinatarajiwa kuwauza jumla ya wachezaji saba ili kujinasia huduma za wanasoka Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund na Declan Rice wa West Ham United.

Licha ya kujishughulisha sana katika soko la uhamisho mwishoni mwa msimu uliopita na kujitwalia maarifa ya wanasoka saba, Chelsea wanakeshea pia huduma za mfumaji Haaland na kiungo Rice kwa matumaini kwamba ujio wao utawawezesha kujizolea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21.

Chelsea walitumia zaidi ya Sh35 bilioni kujisuka upya mwanzoni mwa msimu huu kwa kusajili wanasoka sita wakiwemo Timo Werner, Kai Harvertz, Hakim Ziyech, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Ben Chilwell, Silva na kipa Edouard Mendy.

Mbali na Chelsea,vikosi vingine vinavyowahia huduma za Haaland ni Manchester City na Manchester United ambao pia wanafukuzia maarifa ya kiungo matata raia wa Uingereza anayechezea Dortmund, Jadon Sancho.

Japo kwa sasa anauguza jeraha, Haaland ni miongoni mwa wafumaji matata zaidi wanaoibukia kwa sasa katika soka ya bara Ulaya na amefungia waajiri wake jumla ya mabao 17 kutokana na mechi 14 za hadi kufikia sasa msimu huu.

Rice alianzi kuhusishwa pakubwa na Chelsea mwanzoni mwa msimu wa 2018-19 na alikuwa sehemu ya kikosi cha West Ham kilichopokezwa kichapo cha mabao 3-0 na Chelsea katika gozi la EPL mnamo Disemba 21 uwanjani London.

Kati ya wanasoka saba ambao Chelsea itawatema mnamo Januari 2021 ili kujinasia maarifa ya Haaland na Rice ni Marcos Alonso na Antonio Rudiger ambaye amewajibishwa na Chelsea mara moja pekee ligini hadi kufikia sasa muhula huu.

Wachezaji wengine ni Jorginho, Danny Drinkwater, Victor Moses, Andreas Christensen, Ross Barkley ambaye kwa sasa anachezea Everton ya kocha Carlo Ancelotti kwa mkopo.

You can share this post!

Messi atamani kucheza soka Amerika kabla ya kurejea...

WEST HAM YAPIGA EVERTON: Kocha Moyes aangusha waajiri wake...