• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Messi atamani kucheza soka Amerika kabla ya kurejea Barcelona kuwa kocha

Messi atamani kucheza soka Amerika kabla ya kurejea Barcelona kuwa kocha

Na MASHIRIKA

FOWADI na nahodha wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, amesema kubwa zaidi katika maazimio yake kitaaluma ni kusakata soka ya kulipwa nchini Amerika kabla ya kustaafu ulingoni.

Hata hivyo, amefichua kwamba hana uhakika kuhusu mustakabali wake kitaaluma baada ya mkataba wake wa sasa na waajiri wake nchini Uhispania kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Ilivyo, Messi, 33, atakuwa huru kuanza mazungumzo na kikosi chochote kinachopania kutwaa huduma zake kuanzia Januari mwaka huu wa 2021.

Tetesi kuhusu atakakoteua kuelekea baada ya Juni 2021 zimekuwa nyingi tangu awakabidhi Barcelona barua ya kutaka kuondoka uwanjani Camp Nou mnamo Agosti 2020.

Hata hivyo, amekuwa akihusishwa pakubwa na Manchester City ya kocha Pep Guardiola pamoja na Paris Saint-Germain (PSG) ambao kwa sasa wanatarajiwa kumpokeza mikoba Mauricio Pochettino baada ya kumpiga kalamu Thomas Tuchel mnamo Disemba 24, 2020.

Pochettino ambaye pia amewahi kuwanoa Tottenham Hotspur, aliwahi kuchezea PSG kati ya 2001 na 2003.

Messi amehimizwa pia na kiungo mzawa wa Ujerumani na raia wa Ghana, Kevin-Prince Boateng, 33, ajiunge na Napoli ili afuate nyayo zilizoachwa na aliyekuwa jagina wa soka Diego Maradona kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Maradona aliyeaga dunia mnamo Novemba 25 akiwa na umri wa miaka 60, alijivunia misimu ya kuridhisha zaidi katika taaluma yake ya usogora akivalia jezi za Napoli.

Kwa mujibu wa Boateng ambaye kwa sasa anavalia jezi za AC Monza nchini Italia, huu ndio wakati mwafaka zaidi kwa Messi kutangaza maamuzi ya kutua jijini Naples ili kuendeleza kumbukumbu nzuri za Maradona miongoni mwa mashabiki wa Napoli.

“Sijui ambacho nitafanya wala nitakapoelekea hapo baadaye. Nitasubiri hadi mwisho wa msimu japo matamanio yangu yamekuwa ni kucheza soka nchini Amerika na kuonja uhondo wa Major League Soccer (MLS) kabla ya kurejea Barcelona katika ngazi ya ukocha,” akasema Messi katika mahojiano yake na runinga ya La Sexta nchini Uhispania.

“Hata hivyo, muhimu zaidi kwa sasa ni kumakinikia kikosi cha Barcelona, kukiongoza kukamilisha kampeni za La Liga katika nafasi nzuri na kutwaa mataji bila ya kuathiriwa na tetesi nyingi kuhusu mustakabali wangu kitaaluma,” akaongeza.

Barcelona ambao hawakushinda taji lolote msimu jana, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la La Liga, huu ukiwa mwanzo mbaya zaidi kwao ligini katika kipindi cha miaka 33 iliyopita.

Tangu ajiunge na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13, Messi ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa miamba hao. Aidha, amenyanyua mataji 10 ya La Liga, manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na sita ya Ballon d’Or – tuzo ambayo hutolewa kwa Mchezaji Bora duniani.

Hatua yake ya kuwasilishia Barcelona ombi la kutaka kubanduka ugani Camp Nou mnamo Agosti mwaka huu kulimchochea rais wa kikosi hicho, Josep Maria kujiuzulu mnamo Oktoba, 2020.

You can share this post!

Covid-19 yaunyima mwaka 2021 makaribisho ya haiba

Chelsea kuuza wanasoka saba mwezi huu wa Januari 2021 kwa...