• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
WEST HAM YAPIGA EVERTON: Kocha Moyes aangusha waajiri wake wa zamani

WEST HAM YAPIGA EVERTON: Kocha Moyes aangusha waajiri wake wa zamani

Na MASHIRIKA

TOMAS Soucek alifunga bao katika dakika za mwisho wa kipindi cha pili na kuwasaidia waajiri wake West Ham United kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Ijumaa usiku ugani Goodison Park.

Goli hilo la Soucek lilikuwa zao la krosi iliyochanjwa na Aaron Cresswell kabla ya mpira kumbabatiza kiungo mvamizi wa Everton, Yerry Mina katika dakika ya 85.

Ushindi wa West Ham uliwezesha masogora wa kocha David Moyes aliyewahi kudhibiti mikoba ya Everton kukomesha rekodi ya matokeo mabaya yaliyowashuhudia wakipoteza jumla ya michuano minne mfululizo hapo awali.

Everton walijibwaga ugani kwa minajili ya mchuano huo wakijivunia motisha ya kuibuka na ushindi katika msururu wa mechi nne zilizotangulia na alama tatu dhidi ya West Ham zingaliwapaisha kwenye msimamo wa jedwali la EPL hadi nafasi ya pili kwa alama 32 nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi, Liverpool.

Chini ya mkufunzi Carlo Ancelotti, Everton walipepetana na West Ham wakijivunia kufungwa mara moja pekee kutokana na mechi nne za awali. Kwa upande wao, West Ham walishuka dimbani wakilenga kujinyanyua baada ya Southampton kuwalazimishia sare tasa mnamo Disemba 29, 2020.

Mbali na Soucek aliyefunga bao lake la tano la msimu kufikia sasa ligini, mwanasoka mwingine wa West Ham aliyejituma zaidi dhidi ya Everton ni mshambuliaji Michail Antonio aliyemfanyiza kipa Jordan Pickford kazi ya ziada katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

West Ham walisajili ushindi wao wa tatu ugenini kutokana na mechi tano zilizopita licha ya kukosa huduma za beki Ryan Fredericks na kipa mzoefu Lukasz Fabianski ambaye nafasi yake ilitwaliwa na Randolph. Kikosi hicho cha Moyes kwa sasa kinakamata nafasi ya 10 jedwalini kwa alama 26 sawa na Southampton, Manchester City, Chelsea na Tottenham Hotspur.

Everton ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini, walitumia mchuano huo dhidi ya West Ham kumwajibisha kiungo raia wa Colombia, James Rodriguez kwa mara ya kwanza tangu Disemba 5, 2020 alipopata jeraha la goti.

Everton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Rotherham kutoka Ligi ya Daraja la Pili kwenye mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 9, 2021 huku West Ham wakiwaendea Stockport County kwa minajili ya gozi hilo la Kombe la FA mnamo Januari 11, 2021.

You can share this post!

Chelsea kuuza wanasoka saba mwezi huu wa Januari 2021 kwa...

Watumiaji mitandao ya kijamii wafurahia mvua siku ya kwanza...