• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Chelsea, Liverpool ni kisasi tu fainali ya FA

Chelsea, Liverpool ni kisasi tu fainali ya FA

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

CHELSEA na Liverpool watalenga kulipizana kisasi watakapomenyana katika fainali ya Kombe la FA hii leo. Wote watajibwaga uwanjani Wembley wakiwa na motisha baada ya kuzoa ushindi ligini katikati mwa juma.

Chelsea ya kocha Thomas Tuchel ilipepeta Leeds 3-0 Jumatano kupitia mabao ya Mason Mount, Christian Pulisic na Romelu Lukaku. Liverpool ya kocha Jurgen Klopp ililima Aston Villa 2-1 Jumanne kwa magoli ya Joel Matip na Sadio Mane baada ya Villa kutangulia kufunga kupitia kwa Douglas Luiz.

Mabingwa mara nane wa FA, Chelsea, wanawinda taji lao la kwanza la FA tangu 2018.

Nao Liverpool walitawala mashindano haya mara ya saba na ya mwisho 2006.Chelsea hawana ushindi katika mechi tatu mfululizo dhidi ya Liverpool katika mashindano yote, kwa hivyo wataanza kama wanyonge.

Walilemewa na Liverpool 11-10 kwa njia ya penalti katika fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 27.

Hata hivyo, mara ya mwisho walikutana kwenye dimba la FA mnamo Machi 2020 Chelsea waling’aria Liverpool 2-0 katika raundi ya 16-bora.

Kombe la FA ni shindano pekee Klopp hajashinda Uingereza tangu aajiriwe ugani Anfield mwaka 2015, kwa hivyo analimezea mate sana.

Chelsea nayo itatumai kumaliza nuksi ya kupigwa na Arsenal na Leicester katika fainali mbili zilizopita.

Atakayenyakua taji hilo kati ya Klopp na Tuchel atakuwa kocha wa kwanza Mjerumani kufanya hivyo.

Macho yatakuwa kwa washambulizi Mane na Mount katika mechi hiyo. Liverpool itakosa huduma za kiungo Fabinho nayo Chelsea inatoka jasho kuhusu jeraha la kiungo Mateo Kovacic.

Washindi watapokea kombe pamoja na Sh481.8 milioni nao nambari mbili Sh354.2 milioni.Vikosi vitarajiwa (wachezaji 11 wa kwanza): Chelsea – Edouard Mendy (kipa); Cesar Azpilicueta, Thiago Silva, Antonio Rudiger, Reece James, Jorginho, N’Golo Kante, Marcos Alonso, Mason Mount, Kai Havertz na Timo Werner; Liverpool – Alisson (kipa); Trent Alexander-Arnold, Ibrahima Konate, Virgil van Dijk, Andy Robertson, Fabinho, Thiago Alcantara, Naby Keita, Mohamed Salah, Sadio Mane na Luis Diaz.

  • Tags

You can share this post!

Nunueni chanjo kutoka Afrika, Ramaphosa ashauri

Magharibi, Pwani na Mashariki kuamua mrithi wa Rais Uhuru

T L