• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Nunueni chanjo kutoka Afrika, Ramaphosa ashauri

Nunueni chanjo kutoka Afrika, Ramaphosa ashauri

NA MASHIRIKA

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amezitaka nchi za Magharibi kununua chanjo ya corona itakayotengenezwa katika nchi za Afrika, ikiwemo Kenya.

Ramaphosa alisema kuwa chanjo hiyo huenda ikakosa soko iwapo nchi za nje ya Afrika zitakosa kuinunua.

“Mashirika ya kimataifa ambayo yalipewa pesa nyingi za kununua chanjo kwa ajili ya nchi maskini hayanunui chanjo zilizotengenezwa Afrika, hata zile chanjo ambazo zinatumwa kwa nchi za Afrika,” Ramaphosa aliasema alipokuwa akihutubia mkutano wa kimataifa kuhusu ugonjwa wa corona kwa njia ya mtandao.

Kampuni kubwa ya Afrika Kusini ya kutengeneza dawa Aspen, wiki iliyopita ililalamika kwamba haijapata zabuni yoyote ya chanjo ya corona iliyotengenezwa Afrika kwa ajili ya Afrika, ambayo iliidhinishwa na kampuni ya Amerika Johnson & Johnson, na kutishia kufunga kiwanda chake cha uzalishaji kwa kukosa zabuni.

“Hali hii lazima ikome,” Ramaphosa alisema katika hotuba yake kwa mkutano huo wa pili wa kimataifa kuhusu corona ambao uliongozwa na Rais wa Marekani Joe Biden.

Kampuni ya Aspen ilikuwa ya kwanza kuzalisha chanjo ya corona barani Afrika.Kenya ni miongoni mwa nchi sita za Afrika ambazo zimeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya corona.

Nchi nyingine ambazo zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutengeneza chanjo ya corona inayotumia teknolojia ya mRNA ni Misri, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia.

Nchi hizo zilituma maombi ya kupata teknolojia inayohitajika kuzalisha chanjo ya mRNA Aprili 2021.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliidhinisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chanjo ya Moderna miezi miwili iliyopita.Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya dozi milioni 500 za chanjo kila mwaka.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa miongoni mwa viongozi walioshinikiza Bara la Afrika kujizalishia chanjo ya corona, alitoa hakikisho la kuendelea kushirikiana na washikadau mbalimbali katika sekta ya afya.

“Kupambana na janga la corona katika miaka miwili iliyopita ilitukumbusha kazi ambayo lazima ifanywe ili kuhakikisha usawa wa afya ulimwenguni. Moderna ina dhamira ya kuwa sehemu ya suluhisho,” alisema wakati huo, mtendaji wa kampuni ya Moderna, Stephane Bancel.

Moderna imesema inatumai kutumia kiwanda hicho kugawa dozi za chanjo ya corona kwa mataifa ya Afrika kufikia 2023.

Kwa sasa ni asilimia moja tu ya chanjo zinazotumiwa na nchi za Afrika zinazozalishwa barani Afrika.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Februari mwaka huu, alitangaza kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ipo mbioni katika jitihada za kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo ya corona ili kuokoa fedha nyingi ambazo taifa hilo linazitumia katika kununua chanjo.

Wataalamu wanasema kuwa Bara la Afrika limepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya janga la corona, idadi ya wagonjwa na vifo imepungua.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu (UNITAID), hata hivyo, linasema kuwa janga hilo halifai kupuuzwa.

You can share this post!

Juventus pazuri kuipiku PSG, Real kunasa Pogba

Chelsea, Liverpool ni kisasi tu fainali ya FA

T L