• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Chelsea na Tottenham watoshana nguvu katika gozi la EPL lililotawaliwa na hisia kali

Chelsea na Tottenham watoshana nguvu katika gozi la EPL lililotawaliwa na hisia kali

Na MASHIRIKA

KIZAAZAA na hisia kali zilizotamalaki pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kati ya Chelsea na Tottenham Hotspur ugani Stamford Bridge mnamo Jumapili zilipandisha joto katika hatua za mapema za kampeni za kipute hicho muhula huu wa 2022-23.

Mechi hiyo iliyokamilika kwa sare ya 2-2 na wakufunzi wa pande zote kuonyeshwa kadi nyekundu, ilikuwa jukwaa la Thomas Tuchel wa Chelsea na Antonio Conte wa Spurs kupimana ubabe, kulipizana kisasi na kuendeleza uhasama kati ya vikosi hivyo vya jiji la London.

Makocha wa timu hizo zinazopigiwa upatu wa kutawala soka ya Uingereza na bara Ulaya msimu huu, walianza kuvurugana baada ya Chelsea kuwekwa kifua mbele na beki mzoefu Kalidou Koulibaly kunako dakika ya 19.

Hasira zaidi zilichochewa na refa Anthony Taylor ambaye kwa mujibu wa Tuchel, “alinyima kikosi chake mikwaju kadhaa ya penalti na kupendelea Spurs waliokosa kuadhibiwa licha ya kucheza rafu”.

Bao la pili la Chelsea waliowahi kutwaa taji la EPL na Kombe la FA chini ya Conte mnamo 2017 na 2018, lilifumwa kimiani na Recce James huku Spurs waliotoka nyuma mara mbili wakifunga magoli yao kupitia Pierre-Emile Hojbjerg na Harry Kane.

Tuchel sasa atakosa mchuano ujao wa EPL kati ya Chelsea na Leeds United wikendi hii ugani Elland Road huku adhabu ya Conte ikitarajiwa kumnyima uhondo wa gozi litakalokutanisha waajiri wake na Wolverhampton Wanderers.

Chelsea walianza msimu kwa kupepeta Everton 1-0 ugani Goodison Park huku Spurs wakifungua kampeni zao ligini kwa kukomoa Southampton 4-1 mbele ya mashabiki wa nyumbani. Sawa na Chelsea, Spurs wanatarajiwa pia kutamba msimu huu baada ya kujishughulisha pakubwa katika soko la uhamisho wa wachezaji.

Huku Spurs wakijisuka upya kwa kusajili Destiny Udogie, Fraser Forster, Yves Bissouma, Djed Spence, Clement Lenglet, Ivan Perisic na Richarlison Andrade; Chelsea wameimarisha ngome yao kwa kununua fowadi Raheem Sterling, kiungo Carney Chukuemeka na mabeki wawili – Marc Cucurella na Koulibaly.

“Vikosi vyote vina mseto wa chipukizi na wanasoka wazoefu wenye tajriba pevu na kila mkufunzi ana kiu ya kuwapa mashabiki ‘kitu’ cha kufuatilia msimu huu,” akasema kiungo wa zamani wa Chelsea, Gus Poyet.

Spurs walijibwaga ulingoni wakilenga kuangusha Chelsea ligini kwa mara ya kwanza tangu 2018 na kulipiza kisasi dhidi ya kikosi kilichowadengua kwenye nusu-fainali ya Carabao Cup kwa mabao 3-0 na kuwafunga jumla ya magoli 5-0 katika mikondo miwili ya EPL msimu jana.

Hadi waliposhuka dimbani kuumiza nyasi za Stamford Bridge, Chelsea walikuwa wakijivunia rekodi ya kushinda Spurs mara tano mfululizo katika mashindano ya vipute tofauti.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Je, ni ushirikina, laana au ugonjwa?

Hakuna Rais Mteule nchini kwa sasa, asema Raila

T L