• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
Chelsea pembamba katika UEFA baada ya Real kuwatandika katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ugani Stamford Bridge

Chelsea pembamba katika UEFA baada ya Real kuwatandika katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ugani Stamford Bridge

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Chelsea kuhifadhi taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu yalididimizwa na Real Madrid kwa kichapo cha 3-1 katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali mnamo Jumatano usiku ugani Stamford Bridge.

Kocha Carlo Ancelotti wa Real alikuwa akirejea ugani Stamford Bridge kwa mara ya kwanza tangu aongoze Chelsea kunyanyua taji la Ligi Ku ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA.

Mshambuliaji matata raia wa Ufaransa, Karim Benzema aliwafungulia Real ukurasa wa mabao katika dakika ya 21 kabla ya kufanya mambo kuwa 2-0 kunako dakika ya 24. Ingawa Kai Havertz alirejesha Chelsea mchezoni kwa kuwafungia bao katika dakika ya 40, Benzema alipachika wavuni bao la tatu la Real mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Benzema, 34, alifunga mabao matatu dhidi ya Chelsea siku chache baada ya kufungia Real mabao mengine matatu dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) katika hatua ya 16-bora ya UEFA.

Chelsea sasa watarudiana na Real uwanjani Santiago Bernabeu kwa mkondo wa pili wa robo-fainali mnamo Aprili 12, 2022 wakiwa na mlima mrefu wa kukwea.

Havertz ndiye alifungia Chelsea bao la pekee na la ushindi katika fainali ya UEFA dhidi ya Manchester City mnamo 2020-21. Kipa Edouard Mendy ambaye kwa kawaida huwa tegemeo kubwa la Chelsea, alifanya masihara mara mbili na kumpokeza Benzema nafasi murua za kumwacha hoi katikati ya lango.

Juhudi za kocha Thomas Tuchel kuleta uwanjani wanasoka Mateo Kovacic, Hakim Ziyech na Romelu Lukaku katika kipindi cha pili hazikufua dafu.

Ushindi wa Real unaweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za msimu huu wakijivunia mataji mawili kapuni mwao kadri wanavyofukuzia ubingwa wa UEFA kwa mara ya 14 katika historia.

Kikosi hicho kwa sasa kinaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 69 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na Barcelona, Sevilla na mabingwa watetezi Atletico Madrid. Zimesalia mechi nane pekee kwa kampeni za La Liga kutamatika rasmi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Masharti makali ya IMF kuathiri Wakenya bajeti ikisomwa leo

Jezi ya ‘Hand of God’ ya Maradona sasa kupigwa...

T L