• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Chelsea sasa macho ni kwa FA na UEFA

Chelsea sasa macho ni kwa FA na UEFA

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Thomas Tuchel ametaka masogora wake wa Chelsea kuwa kikosi kitakachoogopwa na kila mshindani katika hatua zilizosalia za kampeni za Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kadri wanavyolenga kutia kapuni mataji ya vipute hivyo muhula huu.

Chelsea walitinga hatua ya nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Jumamosi usiku baada ya kupokeza Middlebrough kichapo cha 2-0 ugani Riverside.

Mabao yao yalifumwa wavuni na Hakim Ziyech na Romelu Lukaku ambaye sasa anajivunia mabao 12 kutokana na mashindano yote msimu huu.

Middlesbrough walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuangusha miamba wengine wa soka ya Uingereza baada ya kudengua Manchester United na Tottenham Hotspur katika hatua za awali za kampeni ya Kombe la FA.

Chelsea walijibwaga ugani dhidi ya Middlesbrough siku moja baada ya kutiwa katika zizi moja na Real Madrid ya Uhispania kwenye robo-fainali za UEFA. Katika safari yao ya kutinga nusu-fainali ya Kombe la FA, Chelsea walizamisha Chesterfield (5-1), Plymouth Argyle (2-1) na Luton Town (3-2) katika raundi za tatu, nne na tano mtawalia.

Iwapo watabandua Real ambao ni wafalme mara 13 wa kivumbi hicho, Tuchel ataongoza kikosi chake kuvaana ama na Atletico Madrid ya Uhispania au watani wao katika EPL, Manchester City, kwenye nusu-fainali.

Mechi dhidi ya Real itakutanisha Chelsea na mkufunzi wao wa zamani, Carlo Ancelotti, aliyewashindia taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA kati ya 2009 na 2011.

“Azma yetu ni kuwa timu ambayo kila mmoja ataomba asikutane nayo katika hatua zilizosalia za Kombe la FA na UEFA msimu huu. Zaidi ya kuhifadhi taji la UEFA, tunalenga pia kunyanyua Kombe la FA kwa kuwa ubingwa wa EPL umetuponyoka,” akasema kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain (PSG).

Kufikia sasa, Chelsea wako katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 59 huku pengo la pointi 11 likitamalaki kati yao na viongozi na mabingwa watetezi Man-City.

Liverpool ni wa pili kwa alama 69 nao Arsenal wanafunga orodha ya nne-bora kwa pointi 54.

Huku nusu-fainali za Kombe la FA zikichezewa ugani Wembley kati ya Aprili 16-17, mechi za mkondo wa kwanza wa robo-fainali za UEFA zitafanyika kati ya Aprili 5-6 na marudiano kuandaliwa Aprili 12-13. Michuano ya mkondo wa kwanza wa nusu-fainali itasakatwa Aprili 26-27 kisha marudiano kufanyika Mei 3-4.

Fainali itapigiwa uwanjani Stade de France jijini Paris. Ilihamishwa kutoka St Petersburg kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Chelsea na Real waliwahi kukutana kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo 2020-21 na vijana wa Tuchel wakabandua miamba hao wa Uhispania kwa jumla ya mabao 3-1 kabla ya kutandika Man-City 1-0 kwenye fainali. Chelsea hawajawahi kupoteza dhidi ya Real kutokana na mechi tano zilizopita.

You can share this post!

Wanawake 4 wajitokeza kumenyania ubunge Kaunti ya Laikipia

Nassir ana nafasi nzuri kumrithi Joho, utafiti waonyesha

T L