• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Chelsea wapepeta RB Salzburg ya Austria na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA

Chelsea wapepeta RB Salzburg ya Austria na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA

Na MASHIRIKA

GRAHAM Potter alikuwa mwingi wa sifa kwa kikosi cha Chelsea kilichoweka kando maruerue ya kupoteza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu na kufuzu kwa hatua ya 16-bora hatimaye baada ya kupepeta RB Salzburg 2-1 mnamo Jumanne usiku nchini Austria.

Mabao mawili kutoka kwa Mateo Kovacic na Kai Havertz yalikomesha rekodi nzuri ya kutopigwa kwa Salzburg katika mechi 40 katika uwanja wao wa nyumbani. Ushindi wa Chelsea uliwashuhudia wakiungana na Manchester City ambao pia ni wawakilishi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Kichapo cha 4-0 ambacho Dinamo Zagreb walipokezwa na AC Milan 4-0 katika mchuano mwingine wa Kundi E mnamo Jumanne kilimaanisha kwamba hakuna uwezekano wa Chelsea kudenguliwa kileleni.

Chelsea walifungua kampeni zao za Kundi E kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Zagreb ya Croatia mnamo Septemba 6, 2022 na matokeo hayo yakachangia kupigwa kalamu kwa kocha Thomas Tuchel siku moja baadaye.

Tangu siku hiyo, Chelsea wamejibu kichapo hicho kwa kushinda michuano mitatu na kuambulia sare mara moja chini ya kocha Potter aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Tuchel.

Chini ya Potter, Chelsea kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya tisa zilizopita licha ya miamba hao wa Uingereza kukosa huduma za wanasoka matata N’Golo Kante, Wesley Fofana, Reece James na Kalidou Koulibaly.

Salzburg walisawazisha kupitia kwa Junior Adamu mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya Kovacic kuwaweka Chelsea kifua mbele katika dakika ya 23. Hata hivyo, Havertz alihakikisha kwamba waajiri wake wanajikatia tiketi ya hatua ya 16-bora kwa kufunga goli la ushindi katika dakika ya 64.

Chelsea kwa sasa wanajivunia alama 10 kutokana na mechi tano za UEFA katika Kundi E, tatu zaidi kuliko nambari mbili AC Milan huku kila kikosi kikisalia na mechi zaidi ya makundi. Salzburg wanajivunia alama sita huku Zagreb wakivuta mkia kwa pointi nne.

Potter kwa sasa anajiandaa kuongoza Chelsea kuveena na waajiri wake wa zamani, Brighton, katika pambano la EPL litakalowakutanisha ugani Amex mnamo Oktoba 29, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Ali Attas

Magavana Pwani sasa wakubaliana kufufua jumuiya

T L