• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
GWIJI WA WIKI: Ali Attas

GWIJI WA WIKI: Ali Attas

NA CHRIS ADUNGO

ALI Attas ni mwandishi mtajika ambaye alikulia jijini Mombasa. “Mombasa ni kitovu cha maisha yangu. Imenilea kimwili na kiakili.”

Safari yake ya elimu ilipitia shule ya msingi ya Serani, shule ya upili ya Khamis na shule ya sekondari ya juu, Allidina Visram.

Tangu utotoni shuleni, aliwika katika masomo ya lugha na Hisabati, akaishia kusomea Lugha, Fasihi ya Kiingereza na Kiswahili na Isimu ya Lugha katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Mmoja kati ya walimu wake mashuhuri alikuwa Profesa Ngugi wa Thiong’o.

Attas aliwahi kufundisha Kiswahili katika shule ya upili ya Aga Khan Academy, Parklands, Nairobi kabla ya kujiunga na Oxford University Press (OUP) kuwa mhariri. Alihariri kazi za waandishi maarufu, akiwemo Profesa Ibrahim Hussein (Arusi, 1980) na akahitimisha kuchapishwa kwa ‘Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la Kwanza’ (1981).

“Nilitunukiwa fahari kubwa kumpelekea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere, nakala ya kwanza ya kamusi hiyo katika Ikulu jijini Dar es Salaam,” anasema.

Miaka michache baadaye, Attas alihamia gazeti la chama tawala zama hizo, ‘Kenya Leo’ (Kenya Times Group) kuwa Naibu Mhariri na akapanda cheo kuwa Mhariri Msimamizi.

Katikati ya mwaka 1986, aliajiriwa na Shirika la Habari la BBC jijini London kuwa mtangazaji, mtafsiri wa habari na mshiriki wa vipindi mbalimbali, kikiwemo ‘Yaliyosemwa na Magazeti ya Afrika Wiki Hii’.

Alihudumu huko kwa miaka minane na nusu kabla ya kuvuka ng’ambo tena na kujiunga na Radio Japani (NHK) jijini Tokyo kuwa mtangazaji na mtafsiri wa habari. Amekuwa pia mtangazaji huria wa Idhaa za Kiswahili za Deutsche Welle (DW) Ujerumani na BBC.

Baada ya kuhitimisha mkataba wake NHK, alipata nafasi ya kuwa mhadhiri wa Kiingereza katika Chuo Kikuu maarufu cha Waseda, Japani. Muda mfupi baadaye, alipata kazi nyingine yenye tunu katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni nchini Japani, akafundisha Kiswahili na Kiingereza kwa zaidi ya miaka ishirini.

Ingawa alistaafu mwaka wa 2021, bado amezama katika kazi za ubunifu wa fasihi tangu ajitose katika uandishi wa kazi bunilizi miaka saba iliyopita. Anajivunia kuandika zaidi ya hadithi 20 za watoto. Ametunga pia ‘Kamusi Mwafaka’ (Moran, 2016) na akawa mmoja wa waandishi sita wa ‘Kamusi Elezi’ (JKF, 2016).

Tamthilia yake ‘Mabandia’ (OUP, 2019) ilifundishwa katika Chuo Kikuu cha Kibabii huku ‘Siwa’ (Moran, 2018) ikifundishwa kwa sasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Tungo zake za ubunifu anasema, zimefaidika kutokana na uzoefu wake wa kazi maishani. Ustadi wake unajidhirisha katika mazungumzo ya tamthilia anazozidi kufyatua. Uchoraji picha halisi wa dhana za hadithi zake sisimuzi unaonyesha upekee wake katika ulingo wa utunzi na ufundi wa kutumia ala za fasihi kusawiri taratibu mbalimbali za maisha ya wanajamii.

Baadhi ya hadithi zake maarufu ni ‘Nguva wa Shimoni’ (2017), ‘Sokwe wa Milima ya Mwezi’ (2017), ‘Miujiza ya Majini’ (2017) na ‘Pepo za Mizimu’ (2017). ‘Fumbo la Watamu’ (2018) ni kitabu chake cha hadithi kilichoibuka cha kwanza katika kategoria ya watoto kwenye Tuzo za Fasihi za Jomo Kenyatta/Wahome Mutahi 2022.

Kazi zake nyingine ambazo zimetajirisha fasihi ya Kiswahili ni ‘Lango La Ajabu’ (2018), ‘Masaibu ya Mosi na Pili’ (2019), ‘Tando la Tandabui’ (2019) na ‘Mbweha Pacha’ (2019). Pia ametunga mfululizo wa hadithi tatu (2020), ‘Ndoto za Juma na Binti’‘Sakata za Juma na Bintiheri’ na ‘Masaibu ya Juma na Bintiheri’.

Vilevile, ametafsiri hadithi mashuhuri nchini Japani, ‘Watoto wa Hiroshima’ (2016) – tafsiri ya insha za kumbukumbu ya maafa ya mabomu ya atomiki yaliyodondoshwa Hiroshima na Nagasaki nchini Japani.

Mwaka huu, Attas ametafsiri kazi maarufu sana duniani –  hadithi ya ‘Mualkemia’ (Moran Publishers, 2022) kutoka kazi asilia ‘The Alchemist’ – riwaya ya mwandishi mtajika Paulo Coelho. Anaungama kuwa uanahabari ulichangia pakubwa kumnoa katika taaluma ya tafsiri.

“Ilinichukua miezi mitatu kutafsiri kitabu hiki ambacho kimetafsiriwa katika zaidi ya lugha 80 na kuuzwa kwa mamilioni nyingi mno kushinda kitabu chochote duniani (kinashikilia rekodi ya dunia katika Guinness World Records).”

“Niliguswa sana na maudhui ya hadithi yenyewe. Inahimiza kila binadamu mwenye maono kujizatiti na kukiuka vizingiti hadi kuizimua ndoto yake ya maisha. Mtu akitia nia, basi atapata njia ya kufanikisha malengo yake,” Attas anaelezea.

“Ni hadithi ya kuvutia ambayo imesomwa na watu wengi duniani, akiwemo Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Ni kazi iliyonipa fursa nyingine ya kuoanisha kipaji cha utunzi na tafsiri katika kuchangia ukwasi wa taaluma ya tafsiri,” anasisitiza.

You can share this post!

USHAURI NASAHA: Katika elimu na maisha mtu hutiwa makali na...

Chelsea wapepeta RB Salzburg ya Austria na kufuzu kwa hatua...

T L