• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Chelsea wapewa Real Madrid katika robo-fainali ya UEFA

Chelsea wapewa Real Madrid katika robo-fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Chelsea watakutana na wafalme mara 13 wa kipute hicho, Real Madrid katika hatua ya robo-fainali msimu huu.

Manchester City watavaana na Atletico Madrid ya Uhispania huku Liverpool ambao pia ni wawakilishi wa soka ya Uingereza wakimenyana na Benfica kutoka Ureno. Miamba wa Ujerumani, Bayern Munich wametiwa katika zizi moja na Villarreal ya Uhispania inayonolewa na kocha wa zamani wa Arsenal na Paris Saint-Germain (PSG), Unai Emery.

Katika hatua ya nusu-fainali, mshindi kati ya Chelsea na Real atakutana na yule atakayetamalaki kipute cha mikondo miwili kati ya Atletico na Man-City. Atakayeibuka mshindi wa michuano ya mikondo miwili kati ya Benfica na Liverpool atachuana ama na Villarreal au Bayern.

Mechi za mkondo wa kwanza wa robo-fainali zitafanyika kati ya Aprili 5-6 na marudiano kuandaliwa Aprili 12-13, 2022. Mechi za mkondo wa kwanza wa nusu-fainali zitasakatwa Aprili 26-27 kisha marudiano kufanyika Mei 3-4, 2022.

Fainali ya UEFA msimu huu itafanyika uwanjani Stade de France jijini Paris, Ufaransa baada ya kuhamishwa kutoka St Petersburg, Urusi kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Ina maana kwamba Chelsea watakutana na kocha wao wa zamani, Carlo Ancelotti aliyewashindia taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA katika kipindi cha miaka miwili ya ukufunzi wake ugani Stamford Bridge kati ya 2009 na 2011.

Mwitaliano huyo ni miongoni mwa wakufunzi watatu pekee kuwahi kushinda taji la UEFA mara tatu, ikiwemo 2014 akidhibiti mikoba ya Real. Alirejea kambini mwa miamba hao wa Uhispania kwa mkondo wa pili mwanzoni mwa msimu huu wa 2021-22 baada ya kuagana na Everton ya Uingereza.

Chelsea na Real walikutana kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo 2020-21 na kocha Thomas Tuchel akaongoza waajiri wake kubandua Real kwa jumla ya mabao 3-1 kabla ya kukomoa Manchester City 1-0 kwenye fainali.

Chelsea hawajawahi kupoteza dhidi ya Real kutokana na mechi tano zilizopita. Atletico wana fursa ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya vikosi vya jiji la Manchester baada ya kukutanishwa na Man-City ya kocha Pep Guardiola. Chini ya mkufunzi Diego Simeone, Atletico walibandua Man-United kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye robo-fainali za UEFA msimu huu.

Itakuwa mara ya kwanza katika historia kwa Atletico kukutana na Man-City waliopokeza Sporting Lisbon kichapo cha jumla ya mabao 5-0 katika robo-fainali na kuweka hai matumaini ya kuzoa taji la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.

Liverpool kwa upande wao wanajivunia kukutana na Benfica mara 10 katika soka ya bara Ulaya, mara ya mwisho zaidi ikiwa katika mechi iliyowavunia ushindi 5-3 katika robo-fainali ya Europa League mnamo 2010.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool wanapigania jumla ya mataji manne muhula huu na tayari wametia kibindoni ubingwa wa Carabao Cup baada ya kupepeta Chelsea kwa penalti 11-10 mwishoni mwa Februari 20222. Kikosi hicho bado kinafukuzia pia Kombe la FA na ubingwa wa EPL.

DROO YA ROBO-FAINALI ZA UEFA 2021-22:

Chelsea vs Real Madrid

Manchester City vs Atletico Madrid

Villarreal vs Bayern Munich

Benfica vs Liverpool

DROO YA NUSU-FAINALI YA UEFA 2021-22:

Man-City au Atletico vs Chelsea au Real

Benfica au Liverpool vs Villarreal au Bayern

You can share this post!

Arsenal wakomoa Villa na kukalia vizuri katika nafasi ya...

Jeraha kumkosesha kipa Ramsdale mechi mbili zijazo za...

T L