• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
Chipukizi Kibet azoa tuzo ya SJAK

Chipukizi Kibet azoa tuzo ya SJAK

NA GEOFFREY ANENE

CHIPUKIZI Aldrine Kibet sasa analenga juu zaidi baada ya kupata motisha ya kuibuka Mwanamichezo Bora wa Agosti katika tuzo ya Chama cha Waandishi Habari za Michezo Kenya (SJAK), mnamo Alhamisi.

Mwanafunzi huyo wa shule ya upili ya wavulana ya St Anthony High Kitale alitwaa tuzo hiyo baada ya kuongoza shule yake kushinda ubingwa wa kitaifa wa soka kwenye Michezo ya Shule za Upili mjini Kakamega mwezi Agosti, ambako pia alitajwa mwanamichezo bora.

Kibet pia aling’ara katika Michezo ya Shule za Upili Afrika Mashariki jijini Kigali, Rwanda, mwezi uo huo.

Tuzo hiyo inadhaminiwa na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG.

Alizawadiwa runinga ya inchi 55 ya thamani ya Sh118,000 madukani kutoka kwa kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG, ambayo ndiyo mdhamini wa tuzo hiyo.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 16 ni mwanafunzi wa pili kupokea tuzo hiyo ya kila mwezi ya LG/SJAK baada ya mshambuliaji wa Gor Mahia, Benson Omalla, aliyetuzwa akiwa katika kidato cha nne katika shule ya Kisumu Day mwaka 2020.

Aidha, ni tineja wa tatu kuzoa tuzo hiyo mbali na Omalla. Mwingine akiwa mwanatenisi Angella Okutoyi ambaye ameishinda mara tatu.

Kibet aliandamana na kocha wake Peter Mayoyo almaarufu Big Machine pamoja na wazazi wake Irene Kwalya na Christopher Komen, kupokezwa tuzo hiyo katika afisi za LG jijini Nairobi, Alhamisi.

Ataelekea nchini Uhispania pamoja na wanafunzi na wanasoka wenza Amos Wamalwa na Alvin Kasavuli kuingia akademia ya Nastic jijini Barcelona.

“Zawadi hii ni motisha kubwa sana kwangu, hasa ninapojiandaa kwenda Uhispania kupalilia talanta yangu. Naahidi kufanya vyema katika taaluma yangu ya soka,” alisema Kibet anayefahamika kwa jina la utani kama Lionel Messi.

Wazazi wake walifurahia tuzo hiyo huku kocha Mayoyo akiongeza kuwa itawapa wanafunzi wengine motisha zaidi kujituma ili wapate pia kutambulika.

Rais wa SJAK James Waindi alisema taifa lina matarajio makubwa kwa Kibet anapoelekea Uhispania.

Afisa wa Mauzo na Mawasiliano wa LG, Maureen Kemunto, aliongeza kuwa inafurahisha kupata mshindi kutoka fani tofauti hasa baada ya wanariadha Beatrice Chebet, Rosemary Wanjiru, Kelvin Kiptum na Faith Kipyegon kutawala tuzo tano kati ya saba za kwanza mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

Polo ahepa demu aliyetaka ‘mpini’ siku ya kwanza

Teknolojia yampiga chenga Linturi Mombasa akitafuta hotuba...

T L