• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
COVID-19: Mechi ya EPL kati ya Tottenham na Arsenal yaahirishwa

COVID-19: Mechi ya EPL kati ya Tottenham na Arsenal yaahirishwa

Na MASHIRIKA

OMBI la Arsenal la kutaka pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililokuwa liwakutanishe na Tottenham Hotspur ugenini mnamo Januari 16, 2022 kuahirishwa limekubaliwa na vinara wa kipute hicho.

Kwa mujibu wa kanuni za EPL, klabu italazimika kucheza mechi iwapo itakuwa na wanasoka 13 na kipa mmoja walio katika hali na uwezo wa kuwajibishwa kambini mwao.

Kikosi cha Arsenal sasa kimesalia hoi kutokana na ongezeko la maambukizi ya visa vya corona pamoja na majeraha. Aidha, baadhi ya wanasoka wao tegemeo wanawakilisha mataifa yao kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Cameroon. Mechi iliyokuwa ikutanishe Spurs na Arsenal sasa ndiyo ya 21 hadi kufikia sasa muhula huu kuahirishwa kwa sababu ya Covid-19.

Mbali na wanasoka Thomas Partey, Mohamed Elneny, Pierre-Emerick Aubameyang na Nicolas Pepe wanaowajibikia nchi zao kwenye AFCON, Arsenal pia wanakosa huduma za wachezaji Cedric Soares, Bukayo Saka na Calum Chambers. Watatu hao walipata majeraha katika mchuano uliopita wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Carabao Cup dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.

Fowadi Martin Odegaard naye ni mgonjwa na kiungo mkabaji Granit Xhaka anatumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Liverpool kwenye mechi iliyopita ya Carabao Cup.

Pambano kati ya Spurs na Arsenal inaahirishwa saa chache tu baada ya jingine lililokuwa likutanishe Burnley na Leicester City kusitishwa kwa sababu ya janga la corona.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sababu ya Aubameyang kukosa mechi ya Gabon dhidi ya Ghana

Mvua kunyesha nchini Januari 15 hadi 19, yasema idara ya...

T L