• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Dereva chipukizi Anwar tayari kupeperusha bendera ya Kenya mbio za magari za dunia

Dereva chipukizi Anwar tayari kupeperusha bendera ya Kenya mbio za magari za dunia

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Mbio za Magari Afrika (ARC) kitengo cha chipukizi Hamza Anwar anasubiri kwa hamu kubwa kuonyesha talanta yake katika Mbio za Magari Duniani za kitengo hicho (JWRC) baada ya kuchaguliwa kushiriki duru zote tano.

Dereva huyo mwenye umri wa miaka 24 atashiriki duru za Uswidi (Februari 9-12), Croatia (Aprili 20-23), Italia (Juni 1-4), Estonia (Julai 20-23) na Ugiriki (Septemba 7-10).

Hamza anayetoka familia ya fani hiyo akiwemo mjombake bingwa mara tatu wa Kenya, Azar Anwar, atapaisha gari la Ford Fiesta R3 kutoka kampuni ya M-Sport Poland.

Dereva huyo alishiriki duru ya Mbio za Magari Duniani (WRC) kwa mara ya kwanza kabisa wakati wa Safari Rally 2021 alipomaliza nambari 25 kwa jumla.

Amekuwa katika mradi wa kukuzwa na Shirikisho la Kimaitafa la Mbio za Magari (FIA Rally Star) tangu 2021 wakati McRae Kimathi aliibuka bingwa wa Afrika wa kitengo cha chipukizi na kushiriki JWRC2022. Kimathi amepitisha umri wa kuwa katika mradi huo ambao ni kati ya 17 na 27. Alikuwa na umri wa 27 mwaka jana.

Hamza atashirikiana na mwelekezi wake Adil Khan kutafuta mafanikio ya JWRC dhidi ya madereva wanane wakiwemo William Creighton na Eamonn (Ireland), Laurent Pellier (Ufaransa), Gregoire Munster (Luxembourg), Tom Rensonnet (Ubelgiji), Diego Dominguez (Paraguay) na Wahispania Raul Hernandez na Roberto Blach.

Hamza, ambaye baba yake Asad Anwar pia ameshiriki mbio za magari za kitaifa kwa miaka mingi, alifurahia fursa ya kushiriki JWRC pamoja na wazo la kuwa dereva wa kulipwa miaka ijayo.

“Tutafanya duru zote tano. Tumeshapewa gari tayari, lakini lazima tutafute wadhamini zaidi kugharamia usafiri na mazoezi ya kabla ya mashindano. Sijawahi kupaisha gari kwenye theluji na ninasubiri kwa hamu kubwa. Lengo langu ni kumaliza mashindano na pia kupata pointi,” alisema mjini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Edwin Sifuna ndiye ‘Musa’ wa kuwakomboa...

WANTO WARUI: Wizara iangazie zaidi vyuo vya ufundi ili...

T L