• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Difenda Raphael Varane akubali kutua Manchester United

Difenda Raphael Varane akubali kutua Manchester United

Na MASHIRIKA

BEKI Mfaransa Raphael Varane ambaye amekuwa akiwajibikia klabu ya Real Madrid, ameafikiana na usimamizi wa Manchester United kuhusu kujiunga na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kima cha Sh5.3 bilioni.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 tayari amewaeleza Real kwamba hana azma ya kurefusha zaidi mkataba wake wa sasa wa mwaka mmoja uwanjani Santiago Bernabeu.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uhispania na Uingereza, uhamisho wa Varane huenda ukafikia Sh6.6 bilioni iwapo vipengele vyote kwenye kandarasi ya sasa ya beki huyo na Real vitazingatiwa kikamilifu.

Kutua kwa Varane uwanjani Old Trafford kutamfanya mchezaji wa pili kusajiliwa na Man-United baada ya kiungo mvamizi Jadon Sancho aliyeondoka Borussia Dortmund kwa Sh11.3 bilioni.

Varane aliingia katika sajili rasmi ya Real mnamo 2011 baada ya kuagana na kikosi cha Lens cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Tangu wakati huo, ameongoza Real kutia kapuni mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia Ufaransa ufalme wa Kombe la Dunia mnamo 2018.

Kufikia sasa, amechezea timu hiyo ya taifa jumla ya mechi 79 na aliwajibishwa mara nne kwenye fainali za Euro 2020 zilizoshuhudia Ufaransa wakibanduliwa na Uswisi kwenye hatua ya 16-bora.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Niko tayari kutetea taji langu la marathon Olimpiki –...

Tundo sasa aongoza jedwali la Mbio za Magari Afrika baada...