• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Edwin Ng’ang’a Thuo: Nahodha anayeinua Mang’u Youth FC

Edwin Ng’ang’a Thuo: Nahodha anayeinua Mang’u Youth FC

Na LAWRENCE ONGARO

MVAMIZI matata wa Mang’u Youth FC Edwin Ng’ang’a Thuo, amethibitisha kuwa ana kipawa maalum.

Chipukizi huyo aligundua kipaji chake cha soka akiwa katika Shule ya Msingi ya Githurai, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Pia chipukizi huyo amethibitisha kuwa ujuzi wake wa soka ulitambulika mwaka wa 2011 alipokuwa katika Kidato cha Kwanza katika Shule ya Upili ya Nyamathumbi, eneo la Gatundu Kaskazini.

Anaeleza kuwa alichangia shule yake kufika katika michezo ya shule za upili eneo la Kati.

“Wakati huo nikicheza kama mshambulizi nikiwa na jezi nambari tisa (9) nilijivunia jumla ya mabao manne katika mashindano hayo,” anaelezea Thuo.

Hapo awali kabla ya kujiunga na Mang’u Youth FC mwaka wa 2019, alikuwa akichezea timu maarufu ya Githurai AllStars Sportiff FC ambayo aliichezea kwa miaka miwili hivi.

Anamtaja kocha wake wa Mang’u Youth Martin Mungai, ambaye ndiye kioo chake kwa sababu amemfanya kuwa na nidhamu ya hali ya juu.

“Unyenyekevu wangu ulimfanya aniteue kama nahodha wa klabu. Hata kikosi kizima cha wachezaji 28 kimefuata mkondo huo,” anasema.

Anasema kutokana na ukakamavu wake akishirikiana na kikosi chake, wanazidi kuongoza Kundi B katika jedwali la ligi ya Central Regional League (CRL) inayoshirikisha timu 11.

Anaeleza amefunga mabao saba (7) kati ya mabao 16 ambayo wamefunga katika mkondo wa kwanza wa ligi.

Timu hiyo imecheza mechi 12 na kushinda tisa (9) huku ikitoka sare kwenye mechi tatu (3) bila kupoteza mechi yoyote. Inajivunia pointi 30 kwa sasa.

Anasifia ligi hiyo kwa sababu imemwezesha kujiepusha na vikundi vya matendo maovu ambayo yangemwingiza katika matendo mabaya.

“Hata hivyo sifa, ninazopata zimeletwa na wachezaji wenzangu watatu ambao ndiyo tunacheza nao safu ya ushambulizi huku tukipokezana pasi za karibu,” anasema.

Chipukizi hao ni Bernard Kairo, Lawrence Njoroge, na Peter Kimani.

Kijana huyu wa miaka 25 analenga kutimiza ndoto yake ya kushiriki soka ya kimataifa.

Anasema kwa sasa timu nyingi zina muandama kutoka kaunti ya Kiambu baada ya yeye kuonyesha ubingwa wake.

“Hata hivyo bado sina haraka yoyote ya kugura kwa sasa lakini bado nataka klabu yangu ya Mang’u Youth ipate ushindi wa ligi msimu huu ili niwe na amani katika nafsi yangu,” alijitetea Nyota huyo.

Kiungo huyo amepania kufika mbali kisoka na hasa ana nia kubwa ya kuhakikisha anavaa jezi ya timu ya Harambee Stars siku za usoni.

“Nafanya bidii na nina matarajio ya kufanikiwa kuwakilisha nchi yangu nyumbani na kimataifa,” anasema mvamizi huyo matata.

Chipukizi huyo anatoa wito kwa vijana wenzake kucheza kandanda ili kuwasha moto talanta zao na kujitahidi kufika mbali.

Anasema ubabe wake wa kufunga mabao mengi umeiwezesha timu hiyo kupata heshima wakiwa bado wanaongoza ligi.

Anataka wanasoka wa mashinani wapewe nafasi kwani wana talanta ya kusakata soka lakini bado hakuna anayewatambua huko.

You can share this post!

Man-United wakomoa Leeds United na kutuma onyo kwa...

Omanyala avunja rekodi 100m Austria