• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Equatorial Guinea yaning’iniza Algeria pembamba kwenye AFCON

Equatorial Guinea yaning’iniza Algeria pembamba kwenye AFCON

Na MASHIRIKA

EQUATORIAL Guinea waliduwaza mabingwa watetezi wa Kombe la Afrika (AFCON), Algeria, kwa kuwapokeza kichapo cha 1-0 katika Kundi E mnamo Jumapili usiku jijini Douala, Cameroon.

Bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na Esteban Obiang katika dakika ya 70. Ushindi huo wa Equatorial Guinea waliokuwa wenyeji wa fainali za AFCON mnamo 2015, sasa unawaning’iniza Algeria padogo huku wafalme hao wa 2019 wakikodolea jicho hatari ya kudenguliwa kwenye hatua ya makundi.

Hakuna nchi ambayo imewahi kutetea ufalme wa AFCON kwa mafanikio tangu Misri wafaulu kufanya hivyo mnamo 2010 baada ya kutandika Ghana 1-0 nchini Angola.

Kufikia sasa, Ivory Coast wanaselelea kileleni mwa Kundi E kwa alama nne, moja zaidi kuliko nambari mbili Equatorial Guinea. Ivory Coast walinyanyua taji la AFCON mnamo 2015 baada ya kupepeta Ghana 9-8 kupitia penalti. Sierra Leone wanakamata nafasi ya tatu kundini kwa pointi mbili huku Algeria wakivuta mkia kwa alama moja pekee baada ya kuambulia sare tasa katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Sierra Leone.

Algeria walishuhudia rekodi yao ya kutoshindwa katika mechi 35 mfululizo ukikatika. Walijitosa ulingoni wakitarajiwa kuendeleza rekodi hiyo na kuweka hai matumaini ya kufikia Italia wanaoshikilia rekodi ya dunia ya kutoshindwa katika mechi 37. Hadi walipozidiwa ujanja na Equatorial Guinea, mara ya mwisho kwa Ivory Coast kutandikwa ilikuwa Oktoba 2018.

Equatorial Guinea wanaonolewa na kocha Juan Micha, walitinga nusu-fainali za AFCON mnamo 2015 walipokuwa wenyeji. Hiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kufuzu kwa fainali za kipute hicho.

Kibarua kigumu zaidi kwa sasa kinachosubiri Algeria ni ulazima wa kushinda Ivory Coast katika mchuano wa tatu na wa mwisho katika Kundi E mnamo Januari 20, 2022 jijini Douala. Equatoria Guinea kwa upande wao watavaana na Sierra Leone jijini Limbe.

Ingawa Algeria wanaonolewa na kocha Djamel Belmadi walikabwa koo katika mchuano wa kwanza wa Kundi E licha ya kushikilia nafasi ya 29 kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Hadi walipozamishwa na Equatorial Guinea, Algeria hawakuwa wamepigwa katika mechi 27 chini ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Walitawazwa wafalme wa makala yaliyopita ya AFCON 2019 baada ya kuwakomoa Senegal 1-0 nchini Misri.

Algeria watakapofunga kampeni zao za Kundi E kwa gozi kali dhidi ya Ivory Coast mnamo Alhamisi, Equatorial Guinea watakuwa wakipimana ubabe na Sierra Leone.

You can share this post!

Refa Alex Kenyani anayepania kuwa kama Mike Dean

Padre afutwa kazi kwa kukataa kuoa

T L