• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Faith Mwende asema yuko ngangari akijiandaa kukwea Mlima Everest

Faith Mwende asema yuko ngangari akijiandaa kukwea Mlima Everest

NA AREGE RUTH

KUKWEA Mlima Kenya inaweza kuwa kazi ngumu kwa watu wengi, lakini kwa hakika si kwa Faith Mwende.

Mwende ambaye ni mchambuzi aliyeidhinishwa wa uwekezaji na fedha, amepanda Mlima Kenya mara tisa; sasa analenga kupanda Mlima Everest ambao una kilele cha juu zaidi duniani cha mita 8,849.

Katika kujiandaa kwa kibarua hicho kikubwa zaidi, Mwende amekuwa akijifua kwa bidii. Ametembea kwenye barafu kubwa amabyo iko kileleni mwa Mlima Kenya huku akiwa amebeba mkoba wenye uzito wa kilogramu 10 mgongoni.

“Lengo langu kuu mwaka huu ni kuwa mwanamke wa kwanza wa Kenya kufika kilele cha Mlima Everest. Niliwahi kupanda kilele cha juu zaidi cha mlima kama huo huko Khumbu, Nepal. Nataka watu wajue faida za kukwea milima,” alisema Mwende kwenye mahojiano katika jumba la Nation Centre mnamo Jumanne.

Katika kauli mbiu yake “Hakuna kilele cha mlima kilicho juu sana”, anatarajia kufikia mafanikio hayo mwezi ujao. Lengo langu kuu la kupanda Mlima Everest ni kusaidia kurejesha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo”.

Faith Mwende akishuka Mlima Everest. PICHA | HISANI

Pia anataka kujenga uelewa juu ya haja ya kuokoa dunia kutokana na uharibifu wa mazingira. Kupitia mpango huo, afisa huyo ambaye pia ni Mwandamizi wa Uzingatiaji katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji, anataka kujenga uelewa juu ya haja ya kushughulikia afya ya akili ya mamilioni ya watu nchini Congo.

Congo kumekuwa kukishuhudiwa vita vya ndani ambavyo vimefanya watu wengi kupoteza maisha yao. Nchi hiyo kwa sasa haina amani.

Wakazi wengi nchini humo wanakimbilia mataifa mengine. Chanzo kuu cha vita hivyo ni kutokana na utajiri wa uchimbaji madini. Ili kuhakikisha kwamba ndoto yake inatimia, Mwende ametimiza ndoto hiyo kwa kukwea milima tofauti tofauti duniani.

Mwende tayari amekwea Mlima Kilimanjaro (Januari), Mlima Rwenzori (Februari 17 hadi 28), na Mlima Kenya (Februari 8 hadi 12). Anapanga safari nyingine ya kupanda Hells Gate, Naivasha mnamo Machi 25 na 26.

Faith Mwende akiwa katika daraja la juu zaidi na kubwa zaidi lililosimamishwa katika mkoa wa Everest lililopewa jina la mtu wa kwanza aliyefikia kilele cha Mlima Everest Sir Edmund Hillary kutoka New Zealand. PICHA | MAKTABA

Mkenya huyo aidha amekuwa akifanya mazoezi na kaka yake mkubwa Stephen Makau na James Kagambi mwenye umri wa miaka 62. Kagambi alikuwa Mkenya wa kwanza kufika kilele cha Mlima Everest mwaka 2022.

“Ndugu yangu pia anapenda kukwea milima sana. Katika familia yetu, sisi wawili tu ndio ambao tunakwea milima pekee. Yeye hunisukuma kufanya kazi kwa bidii kila siku. Wana familia wengine pia huwa wanatupa usaidizi wakati tunahitaji. Wamekuwa wa msaada mkubwa kwetu,” alisema. Mwende

“Nilipoanza kuonyesha nia ya kupanda milima nikiwa na umri wa miaka 12, nilimtegemea baba yangu ambaye alikuwa akitupeleka kwenye pikiniki na hiyo ilinitia moyo kupenda mazingira,” alisema Mwende ambaye alilelewa katika eneo lenye milima la Kilungu katika Kaunti ya Makueni.

Mwende ambaye pia ni muogeleaji na mchezaji wa gofu, amewataka wanawake zaidi kujiunga na tasnia hii ambayo anasema ina manufaa makubwa ya kiafya.

“Mara nyingi ambapo nimepanda milimani, nimekutana na wanaume pekee. Ninawasihi wanawake zaidi kuingia kwenye meli hii ambayo nimekuwa dereva kwa muda mrefu. Ina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kupata utimamu wa mwili na afya ya akili. Mazingira pia yana pendeza, yanatufanya tuhisi tuko karibi zaidi na Mungu,” alisema Mwende.

Alisema ili kufika kilele cha mlima, mtu anahitaji subira, uthabiti na ustahimilivu. Utafiti pia ni muhimu kabla ya kupanda mlima wowote ilikuweza kuelewa mazingira.

Aidha anasema, changamoto kubwa ambayo anapitia ni ukosefu wa fedha za kutosha ambazo zitamsaidia kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya safari hiyo.

Hata hivyo, ameomba waziri wa Michezo Ababu Namwamba kutambua ukweyaji milima kama michezo mingine ile.

“Ningeomba wafadhili kujitokeza kunipa msaada wakati ninapoendelea kujiandaa kwa safarii hii ndefu. Ningeomba pia wizara ya michezo na wadhamini kujitolea kutupa msaada kama wanavyofanya katika michezo mingine,” aliongezea Mwende.

  • Tags

You can share this post!

Raila azindua maasi serikali ikitoa onyo

Shirleen analenga kutamba kinoma katika uigizaji

T L