• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Firat ndiye kocha mkuu wa Harambee Stars

Firat ndiye kocha mkuu wa Harambee Stars

NA JOHN ASHIHUNDU

AFISA Mkuu wa Shirikisho la Kitaifa la Soka (FKF), Barry Otieno amethibitisha kwamba Engin Firat ataendelea kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa – Harambee Stars – baada ya kuondoka ghafla mwezi Novemba 2021.

Otieno alisema baraza kuu la shirikisho hilo limekutana na kuamua kuongeza muda wa mkataba raia huyo wa Uturuki mwenye umri wa 52.

“Tumekutana katikati mwa wiki na kuamua kuurefusha mkataba wa Firat kama kocha wa Harambee Stars,” Otieno alisema huku akiongeza kwamba mkufunzi huyo ataruhusiwa kuteua msaidizi wake bila kushurutishwa.

“Kama kawaida yetu tutampa fursa ya kuteua wasaidizi wake, na bila shaka tunamtarajia kufanye hivyo kwa muda usio mrefu.”

Firat aliyekuwa akifunza timu ya taifa ya Moldova alipewa jukumu hilo siku chache baada ya Jacob ‘Ghost’ Mulee kuondoka mwaka uliopita, wasaidizi wake wakiwa Ken Odhiambo na William Muluya, wakati Fredrick Onyango kama mkufunzi wa mkipa.

Kocha huyo mwenye leseni ya ukufunzi kutoka UEFA aliajiriwa wakati Harambee Stars walikuwa wakishiriki katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia na Stars ilikuwa katika nafasi ya pili kwenye Kundi E.

Alianza kazi kwa kusimamia tmu hiyo dhidi ya Mali katika nyumbani na ugenini Oktoba 8 na 12, 2021, mtawaliwa ambapo Stars ilichapwa 5-0 katika mechi iliyochezewa Agadir Stadium nchini Morocco, kabla ya kuchapwa 1-0 katika mechi ya marudiano iliyochezewa Nyayo Stadium.

Mbali na kuongoza timu ya taifa ya Iran, Firat aliandaa klabu za ligi kuu nchini Iran, zikiwemo Saipa, Folad Tabriz na Sepahan.

Baada ya Firat kuondoka, kamati ya mpito iliyoteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Amina Mohamed ilimteua Alex Alumirah kuwa kocha mkuu wa Harambee Stars, lakini akizungmza na waandishi, Otieno alisema kocha huyo wa zamani wa klabu ya Vihiga Queens hakuteuliwa na FKF.

“Hatuna mkataba wowote na Alumirah, hivyo hatamtambui kama kocha mkuu wa timu ya taifa. Hatuna uhazama wowote naye. Ni kocha mzuri na tungependa kufanya naye kazi siku zijazo.”

Charles Okere alitekeleza wajibu huo wa kocha mkuu wa Stars, kabla ya Alumirah kuteuliwa na kamati ya mpito.

Otieno alisema FKF imeorodhesha mipango ya kufufua timu ya taifa baada ya marufuku ya FIFA kuondolewa majuzi.

Alisema FKF itaanzisha rasmi shughuli za kuunda kikosi cha Harambee Stars kuanzia Februari 2023 kwa lengo la kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) za 2027, huku akiipongeza Serikali kwa kuahidi kuweka kando pesa za kuanzisha kampeni maaluma za kuhakikisha Harambee Stars imefuzu kwa Kombe la Dunia la 2030.

Alisema FKF itahusika vilivyo kwenye kampeni hizo na kuhakikisha soka imeimarika kuanzia mashinani ili kufanikisha lengo hilo.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Croatia walivyoridhika na...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Messi kuendelea kuchezea...

T L