• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Messi kuendelea kuchezea Argentina, kocha wake atamani anogeshe fainali za dunia 2026

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Messi kuendelea kuchezea Argentina, kocha wake atamani anogeshe fainali za dunia 2026

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi amesema hatastaafu soka ya kimataifa baada ya kuongoza Argentina kutawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 36 akivalia utepe wa nahodha.

Fowadi huyo mzoefu wa Paris Saint-Germain (PSG) alifichua hayo katika mahojiano yake na runinga ya Tyc Sports ya Argentina baada ya taifa lake kufunga Ufaransa penalti 4-2 kufuatia sare ya 3-3 kwenye fainali ya Disemba 18, 2022 ugani Lusail Iconic.

Messi atakayefikisha umri wa miaka 36 mwaka ujao, anaamini kuwa angali na mchango mkubwa kitaaluma akivalia jezi za Argentina.

“Napenda soka. Ndicho kitu ninachofanya. Nafurahia kuwa sehemu ya timu ya taifa na natamani kuendelea kutandaza mechi kadhaa za kimataifa nikiwa mshindi wa Kombe la Dunia,” akasema sogora huyo wa zamani wa Barcelona.

“Bila shaka nilitaka pambano dhidi ya Ufaransa katika Kombe la Dunia liwe langu la mwisho kimataifa ili nisitake chochote zaidi,” akaongezea.

Akinogesha fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano katika taaluma yake ya usogora, Messi alipachika wavuni mabao mawili dhidi ya Ufaransa katika fainali ya Jumapili nchini Qatar na akafunga pia penalti wakati wa kutafuta mshindi kupitia matuta.

Ndiye aliibuka mchezaji bora wa makala ya 22 ya fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kupachika wavuni mabao saba na kuchangia krosi tatu zilizozaa mabao.

Messi atakuwa na umri wa miaka 39 fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakapofanyika nchini Amerika, Canada na Mexico.

Hata hivyo, kocha Lionel Scaloni wa Argentina amesema angependa Messi awe sehemu ya kikosi chake wakati wa fainali hizo za dunia mnamo 2026.

“Kwanza kabisa, tunahitaji kumhakikishia nafasi katika kikosi kitakachowakilisha Argentina kwenye makala yajayo ya fainali za Kombe la Dunia,” akatanguliza.

“Iwapo anataka kuendelea kucheza, basi atakuwa pamoja nasi. Ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu mustakabali wake kitaaluma. Ataamua iwapo atasalia kuwa mchezaji wa Argentina au la,” akasema Scaloni kwa kusisitiza kuwa ni fahari tele kuwa kocha wa Messi ambaye huwa mstari wa mbele kuwakuza wanasoka wenzake kikosini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Firat ndiye kocha mkuu wa Harambee Stars

Wito kwa serikali za nchi za Afrika ziongeze uwekezaji...

T L