• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Croatia walivyoridhika na shaba Morocco wakirejea nyumbani kishujaa

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Croatia walivyoridhika na shaba Morocco wakirejea nyumbani kishujaa

Na MASHIRIKA

KOCHA Zlatko Dalic amesema kubwa zaidi katika mipango yake kwa sasa ni kuongoza Croatia kunyanyua ubingwa wa kipute cha Uefa Nations League 2023 na fainali za Euro 2024.

Hii ni baada ya masogora wake kukomoa Morocco 2-1 ugani Khalifa International mnamo Jumamosi na kuzoa nishani ya shaba kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu.

Croatia waliambulia nafasi ya pili duniani mnamo 2018 baada ya Ufaransa kuwapepeta 4-2 jijini Moscow, Urusi. Sasa wamemaliza fainali za Kombe la Dunia ndani ya mduara wa tatu-bora kwa mara ya tatu katika historia. Waliwahi kupepeta Uholanzi 2-1 mnamo 1998 nchini Ufaransa na kujizolea shaba nyingine.

“Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu zilikuwa za mwisho kwa baadhi ya masogora wangu wazoefu akiwemo Luka Modric, 37. Sasa nalenga kusuka kikosi kipya kitakachodumisha uhai wa ndoto ya kutamalaki Nations League 2023 na Euro 2024,” akasema Dalic.

Croatia wanaojivunia mseto wa chipukizi matata na wachezaji wazoefu, watavaana na Italia, Uhispania na Uholanzi kwenye fainali za Nations League mwakani kabla ya kuelekea Ujerumani kwa Euro 2024.

Mabao yao dhidi ya Morocco yalifumwa wavuni kupitia Josko Gvardiol na Mislav Orsic. Morocco waliofutiwa machozi na Achraf Dari, walijibwaga ugani kishujaa baada ya kuweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza cha Afrika kuwahi kutinga nusu-fainali za Kombe la Dunia.

Chini ya kocha Walid Regragui, wafalme hao wa Afrika 1976 waling’olewa na Ufaransa katika nusu-fainali kwa mabao 2-0. Walianza kampeni za Kundi F kwa sare tasa dhidi ya Croatia kabla ya kuduwaza Ubelgiji kwa 2-0 na kupepeta Canada 2-1. Walikomoa Ureno 1-0 katika robo-fainali baada ya kudengua Uhispania kwa penalti 3-0 kufuatia sare tasa katika raundi ya 16-bora.

Croatia walitinga nne-bora baada ya kufunga Brazil penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 katika robo-fainali. Walifunga Japan penalti 3-1 baada ya sare ya 1-1 katika raundi ya 16-bora. Walicharaza Canada 4-1 na kuambulia sare tasa dhidi ya Ubelgiji katika michuano mingine ya Kundi F.

Morocco wanaoorodheshwa wa 22 kimataifa, waliondoka Qatar wakiwa wamefungwa mabao matano pekee na kupoteza mechi mbili kati ya saba.

Hadi walipopigwa breki na Ufaransa kwenye nusu-fainali, hawakuwa wameshindwa katika michuano sita ya Kombe la Dunia tangu Ureno iwalaze 1-0 katika Kundi B mnamo 2018 nchini Urusi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nahodha Luka Modric kuendelea...

Firat ndiye kocha mkuu wa Harambee Stars

T L