• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Fowadi Jordan Larsson aitwa kambini mwa Uswidi kujaza pengo la majeruhi Zlatan Ibrahimovic

Fowadi Jordan Larsson aitwa kambini mwa Uswidi kujaza pengo la majeruhi Zlatan Ibrahimovic

Na MASHIRIKA

KOCHA Janne Andersson wa timu wa taifa ya Uswidi amemteua fowadi Jordan Larsson, 23, kuwa kizibo cha kigogo Zlatan Ibrahimovic katika timu ya taifa itakayotegemewa na Uswidi kwenye fainali zijazo za Euro.

Ibrahimovic aliyerejea katika timu ya taifa mnamo Machi 2021 baada ya kuwa nje kwa takriban miaka mitano, atakosa kuwa sehemu ya kikosi cha Uswidi kutokana na jeraha la goti alilolipata wakati akiwachezea waajiri wake AC Milan dhidi ya Juventus mwanzoni mwa Mei 2021.

Larsson ni mtoto wa mwanasoka nguli Henrik aliyewahi kushirikiana na Ibrahimovic kwenye safu ya mbele ya timu ya taifa ya Uswidi. Larsson hakuunga kikosi cha kwanza cha Uswidi katika mechi zilizopita za kimataifa zilizotandazwa na Uswidi mnamo Machi 2021.

“Hakuwa katika fomu nzuri wakati huo. Isitoshe, nilikuwa tayari na wafumaji wanne tegemeo, akiwemo Ibrahimovic ambaye kwa sasa hatakuwepo. Ndipo nimefikiria kumleta Larsson ambaye ana kasi na ubunifu mkubwa utakaotatiza mabeki wa wapinzani wetu,” akasema Andersson.

Larsson ambaye hutumia sana guu lake la kushoto, anajivunia kufungia kikosi cha Spartak Moscow jumla ya mabao 10 kutokana na mechi 20 zilizopita za Ligi Kuu ya Urusi.

Uswidi wametiwa katika Kundi E kwa pamoja na Uhispania, Slovakia na Poland kwenye fainali zijazo za Euro ambazo zitapigwa kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Kikosi cha kocha Andersson kinajivunia mseto wa wanasoka wazoefu na chipukizi kadhaa, akiwemo Alexander Isak, 21, ambaye amefungia Real Sociedad ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) jumla ya mabao 16 kufikia sasa muhula huu. Kigogo Andreas Granqvist, 36, ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Uswidi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wadai taarifa ya pesa zilizotumika kwa BBI

TAHARIRI: Yafaa Rais aupime ushauri anaopewa