• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Wadai taarifa ya pesa zilizotumika kwa BBI

Wadai taarifa ya pesa zilizotumika kwa BBI

Na WANDERI KAMAU

MASHIRIKA ya kutetea haki za umma yanamtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, kufanya ukaguzi kuhusu fedha zote zilizotumika kwenye mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) tangu ulipoanza.

Mashirika pia yanamtaka Bi Gathungu kuchapisha ripoti ya kina kuhusu zilikotoka fedha hizo, jinsi zilivyotumika na kuitoa kwa umma.

Kwenye taarifa ya pamoja jana, mashirika hayo 16 yalisema kuwa serikali imekuwa ikiendesha mchakato huo kwa njia fiche, bila ya kuwaeleza Wakenya kuhusu kule inakotoa fedha hizo.

Mchakato huo umekuwa ukionekana kuyumba tangu wiki iliyopita, baada ya Mahakama Kuu kuutangaza kuwa haramu, na ulioendeshwa kwa kutozingatia taratibu zifaazo za kisheria.

Uamuzi huo umeonekana kama pigo kubwa la kisiasa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ikizingatiwa wao ndio waliouanzisha, mara tu baada ya handisheki mnamo 2018.

Ikizingatiwa serikali haijakuwa ikiweka wazi kule inakotoa fedha za kuendesha mpango huo, mashirika yalisema Rais Kenyatta anapaswa kuwajibikia fedha zilizotumika.

“Kutokana na uamuzi wa mahakama kuutangaza mpango kuwa haramu, Rais anapaswa kuwajibikia pesa zote za umma ambazo zimekuwa zikitumika kuuendesha,” yakasema.

Baadhi ya mashirika yaliyotoa kauli hiyo ni Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KHRC), Defenders Coalition, Transparency International (TI) Kenya, Independent Medico-Legal Unit (IMLU), Kongamano la Mageuzi kati ya mengine.

Imekuwa ikikisiwa mchakato umemgharimu mlipaushuru zaidi ya Sh10 bilioni, ingawa serikali haijawahi kutoa maelezo kuhusu kiwango halisi cha fedha kilichotumika.

Mashirika hayo pia yalishinikiza taasisi zote za umma—akiwemo Rais, idara za serikali na maafisa wa serikali ya Kitaifa na zile za kaunti kukoma kutumia fedha za umma kuuendesha mchakato huo.

“Maafisa wa serikali wanapaswa kuwatumikia Wakenya, badala ya kushiriki kwenye mchakato ambao hauwafaidi kwa vyovyote vile,” yakasema.

Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa kutumia nguvu kuupigia debe mchakato huo, hasa machifu.

Kwenye zoezi la kukusanya saini za kuunga mkono mpango huo mwaka uliopita, serikali ililaumiwa kuwatumia machifu, manaibu wao, wazee wa vijiji na maafisa wengine wa utawala kuwashinikiza Wakenya kutia saini fomu hizo.

Hata hivyo, Waziri wa Utawala wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alipinga vikali madai hayo, akiyataja kuwa vumi zisizokuwa na msingi wowote.

You can share this post!

Uhuru na Raila kusafiri kwa garimoshi hadi jijini Kisumu

Fowadi Jordan Larsson aitwa kambini mwa Uswidi kujaza pengo...