• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Gambia waanza kampeni za AFCON kwa matao ya juu baada ya kuzamisha Mauritania katika Kundi F

Gambia waanza kampeni za AFCON kwa matao ya juu baada ya kuzamisha Mauritania katika Kundi F

Na MASHIRIKA

GAMBIA walianza vyema kampeni zao kwenye Kombe la Afrika (AFCON) kwa kutandika Mauritania 1-0 katika mchuano wa Kundi F uliowakutanisha mjini Limbe.

Mshambuliaji Ablie Jallow alifungia Gambia bao hilo la pekee na la ushindi katika dakika ya 10 baada ya kushirikiana vilivyo na Musa Barrow.

Ingawa Mauritania walikita kambi kwenye lango la Gambia mwishoni mwa kipindi cha kwanza na mwanzoni mwa kipindi cha pili, juhudi zao ziliambulia pakavu baada ya kushindwa kumzidi ujanja kipa Modou Jobe.

Gambia almaarufu The Scorpions sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi F kwa alama tatu sawa na Mali walioduwaza Tunisia kwa kichapo cha 1-0 katika mchuano mwingine wa Jumatano.

Wakishikilia nambari ya 150 kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gambia ndicho kikosi kinachoshikilia nafasi ya chini zaidi katika fainali za AFCON nchini Cameroon na wameratibiwa kuvaana na Mali katika mechi ijayo ya makundi mnamo Januari 16, 2022.

Miaka 40 baada ya kujaribu kufuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya kwanza bila kufaulu, Gambia hatimaye walifanikiwa kunogesha makala ya 33 ya kipute hicho mwaka huu.

Ushindi wa Gambia dhidi ya Mauritania ni fahari tele zaidi kwa mashabiki wa taifa hilo linalojivunia raia 2.5 milioni pekee. Tija zaidi ni kwa beki Modou Jagne ambaye ni mwanasoka mkongwe zaidi kambini mwa Gambia ikizingatiwa kwamba alichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza mnamo 2006.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alishirikiana vilivyo na Jallow aliyemwacha hoi kipa wa Mauritania, Boubacar Diop katika dakika ya 10.

Mauritania wanaotiwa makali na kocha Didier Gomes Da Rosa aliyepokezwa mikoba miezi miwili iliyopita, walitegemea zaidi maarifa ya fowadi Pape Ibnou Ba anayechezea kikosi cha Le Havre nchini Ufaransa.

Mnamo 2019, Mauritania walikuwa katika hali sawa inayowazingira Gambia kwa sasa. Wakati huo, Mauritania walikuwa wakinogesha fainali za AFCON kwa mara ya kwanza. Walibanduliwa katika raundi ya kwanza baada ya kutosajili ushindi wowote ila wakafunga bao moja na kuambulia sare mara mbili kutokana na mechi tatu za makundi.

Gambia wangalifunga mabao zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila beki wa Sampdoria, Omar Colley pamoja na Ebrima Colley wakapoteza nafasi nyingi za wazi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Gakuyo ahimiza wafuasi wake wafuate ngoma ya Azimio la Umoja

FASIHI SIMULIZI: Utanzu wa Semi na vipera vyake

T L