• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
FASIHI SIMULIZI: Utanzu wa Semi na vipera vyake

FASIHI SIMULIZI: Utanzu wa Semi na vipera vyake

MPENDWA msomaji, leo tutagusia utanzu wa Semi.

Semi ni tungo fupi zinazowasilisha ujumbe kwa kufumba au kuchora picha ili kutoa ushauri kwa wanajamii. Pia huitwa tungo fupi.

VIPERA VYA SEMI

Misemo

Ni fungu la maneno machache linalobeba maana fiche. Hususan huunganisha dhana mbili kuwa moja? Mfano wa misemo:

i) Arusi ya mzofafa – arusi iliyojaa mbwembwe na madoido

ii) Macho ya chawa – kuwa na macho madogo

iii) Shilingi kwa ya pili – kufanana

Nahau

Ni utungo mfupi unaotumia maneno ya kawaida kuibua maana fiche. Huchukua muundo wa kitenzi pamoja na nomino; T + N = Nahau

Mifano

Shika sikio – kataza mtu kutenda mabaya

Tia shime – himiza mtu

Piga ramli – kubashiri/tabiri kama anavyofanya mganga

Misimu au simo

Ni maneno yanayozuka baina ya makundi ya watu wenye uhusiano wa karibu na hutumiwa kimafumbo kati yao pekee. Maneno hayo huzuka na kutoweka baada ya muda mfupi. Hata hivyo, yakidumu husanifishwa na kuwa msamiati wa kawaida wa lugha husika. Mifano ya misimu

Sonko – tajiri

Kufinywa – kudhulumiwa

Jisikia sukari – kuringa

Methali

Ni kauli za kimapokeo ambazo hufumba ujumbe/ushauri kwa njia ya mkato. Huwa na maana ya nje/bayana na maana ya ndani/batini. Mifano ya methali

(i) Mgomba changaraweni haupandwi ukamea

(ii) Lakabu Chiriku mzee hakamatwi kwa makapi

Vitendawili

Ni kauli fupi kwa njia ya maswali zenye maana fiche. Mifano ya vitendawili; Kitendawili? Tega!

i) Aliwa, yuala, ala na aliwa? – papa

ii) Kiti cha dhahabu hakikaliwi na watu? – moto

Shirikina

Tungo zinazobainisha imani tofauti za jamii husika. Kwa mfano; Ukila chakula gizani utakula na shetani.

Bundi akilia karibu na nyumba mtu mmoja wa nyumba ile atafariki. (maneno 305)

Mwandalizi: Mwalimu Borwo Chepkoit

Mkuu wa Idara ya Kiswahili

Shule ya Upili ya Wasichana ya Alliance

  • Tags

You can share this post!

Gambia waanza kampeni za AFCON kwa matao ya juu baada ya...

AFCON: Ivory Coast wakung’uta Equatorial Guinea...

T L