• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Haaland hachoki kufunga, amepachika wavuni mabao 11 kutokana na mechi nane zilizopita

Haaland hachoki kufunga, amepachika wavuni mabao 11 kutokana na mechi nane zilizopita

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland aliendeleza ubabe wake wa kufunga mabao kwa kupachika wavuni magoli matatu katika ushindi wa 5-1 uliosajiliwa na Norway dhidi ya Gibraltar katika mechi ya Kundi G kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Kristian Thorstvedt alifungulia Norway karamu ya mabao katika dakika ya 22 kabla ya kuchangia goli la pili lililofumwa wavuni na Haaland dakika tano baadaye.

Haaland alitikisa nyavu kwa mara ya pili katika dakika ya 39 kabla ya Reece Styche kufanya mambo kuwa 3-1 mwishoni mwa kipindi cha pili.

Alexander Sorloth alifunga bao kunako dakika ya 59 na kurejeshea Norway uongozi wa mabao matatu kabla ya Haaland kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili.

Haaland ambaye ni mchezaji wa Borussia Dortmund, sasa anajivunia mabao 11 kutokana na mechi nane zilizopita katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Kufikia sasa, amefunga mabao matatu katika mechi moja mara mbili, mara ya kwanza ikiwa katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Dortmund dhidi ya Wehen Wiesbaden katika German Cup muhula huu wa 2021-22.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Memphis Depay afunga mabao matatu na kuongoza Uholanzi...

Bernardo Silva na Diogo Jota watambisha Ureno dhidi ya...