• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
Hali ni tete kuhusu mkataba mpya wa Salah kambini mwa Liverpool

Hali ni tete kuhusu mkataba mpya wa Salah kambini mwa Liverpool

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amesema mustakabali wa nyota Mohamed Salah ugani Anfield utategemea maamuzi yake ya ama kutia saini au kukataa ofa ya kandarasi mpya.

“Kila kitu kinamtegemea Salah. Klabu imefanya kila liwezekanalo katika juhudi za kumshawishi kurefusha kandarasi yake. Sidhani kutakuwepo na mjadala zaidi,” akasema Klopp.

Mkataba wa sasa kati ya Liverpool na fowadi huyo matata raia wa Misri anayewaniwa pakubwa na Real Madrid unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao wa 2022-23.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Salah alisema asingetaka kushinikiza waajiri wake “kumpa kitu kisichowezekana” katika mazungumzo kuhusu uwezekano wa Liverpool kurefusha mkataba wake ugani Anfield.

Fowadi huyo wa zamani wa Chelsea na AS Roma atafikisha umri wa miaka 30 mnamo Juni 2022 na amesisitiza kuwa anachotarajia kutoka kwa waajiri wake ni “shukran” kutokana na mambo mengi ambayo amewawezesha miamba kujivunia kutokana na mchango wake kikosini.

“Natamani sana kusalia Liverpool. Wenye uwezo wa kufanya maamuzi hayo ni Liverpool. Sina mamlaka yoyote. Ila nawaomba hisani moja – wanipe shukran kwa yale nimewafanyia. Siulizi kitu kilicho nje ya uwezo wao kutimiza,” akasema.

Salah ambaye sasa amehudumu kambini mwa Liverpool kwa miaka mitano kuanzia 2017, alisaidia kikosi hicho kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2018-19 na 2019-20 mtawalia. Aliongoza Liverpool pia kunyanyua Kombe la Dunia na Uefa Super Cup mnamo 2019 na amefungia waajiri wake mabao 152 kutokana na mechi 237 zilizopita.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nyong’o: Serikali ya Raila itaongezea kaunti mgao wa...

Wito serikali iondoe ada za juu katika viwanja bora...

T L