• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Nyong’o: Serikali ya Raila itaongezea kaunti mgao wa bajeti

Nyong’o: Serikali ya Raila itaongezea kaunti mgao wa bajeti

NA SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga ameendeleza kampeni kusaka kura akilenga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Ijumaa, chini ya vuguvugu la Azimio la Umoja analoongoza, Bw Raila alielekeza ndoano yake katika Kaunti ya Kisumu.

Gavana mwenyeji wa kaunti hiyo, Profesa Anyang’ Nyong’o alitumia jukwaa hilo kuahidi endapo Bw Raila atatwaa uongozi, serikali yake itaongezea serikali za kaunti asilimia 5 juu ya mgao wa fedha ambazo zinazopokea.

Kwa sasa, serikali za kaunti zinapata mgao wa asilimia 15 ya idadi jumla ya makadirio ya bajeti kila mwaka.

Hata hivyo, Katiba inapendekeza kaunti kupokea mgao usiopungua asilimia 35.

“Serikali ya Raila Odinga, itaongezea kaunti asilimia 5 zaidi,” Profesa Nyong’o akasema.

Gavana huyo alisema, nyongeza hiyo itasaidia kufanikisha uboreshaji wa miundomsingi kama barabara, afya bora na kuhakikisha Wakenya wanapata pesa mifukoni.

Alisifia salamu za mapatano, maarufu kama Handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila, Machi 2018, kuletea Kisumu maendeleo.

“Tumepata bandari, maendeleo yaliyojiri kutokana na ushirikiano wa karibu baina ya Rais na Raila,” akaelezea.

Katika kampeni ya Waziri huyo Mkuu wa Zamani Kisumu, alikuwa ameandamana na magavana wa Nyanza wanaojumuisha, Cyprian Awiti (Homa Bay) na James Ongwe wa Kisii.

Wengine ni; Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, Dkt Alfred Mutua (Machakos), na Charity Ngilu wa Kitui.

  • Tags

You can share this post!

Covid-19: Vijana wahimizwa wajitokeze kwa wingi kupata...

Hali ni tete kuhusu mkataba mpya wa Salah kambini mwa...

T L