• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Harambee Stars nje ya safari ya kufika Cameroon kwa AFCON 2022

Harambee Stars nje ya safari ya kufika Cameroon kwa AFCON 2022

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi Kenya imebanduliwa kwenye kampeni yake ya kufika Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2022 baada ya kukosa ushindi iliohitaji dhidi ya Misri katika sare ya 1-1 ugani Kasarani mnamo Alhamisi.

Siku moja baada ya wenzao kutoka eneo la Cecafa Sudan, Ethiopia na Rwanda kuweka matumaini yao ya kufuzu hai baada ya kuchapa Sao Tome & Principe, Madagascar na Msumbiji mtawalia, Stars ilitikiswa na bao la mapema, huku mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Japan mwaka 2020 Michael ‘Engineer’ Olunga akinyamazishwa.

Vijana wa kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee waliingia mchuo huo wao wa tano wa Kundi G wakihitaji ushindi pekee ili kuchelewesha Misri kufuzu.

Hata hivyo, walijipata na mlima mkubwa wa kukwea Mohamed Magdy Mohamed Morsy maarufu Afsha aliposukumia kipa Ian Otieno shuti kali hadi wavuni dakika ya pili ugani Kasarani.

Mambo hayakuwa yakiendea Stars vyema kwani ilipata bao kupitia Masud Juma dakika ya 40, lakini halikusimama kwa sababu ilipatikana mchezaji Mkenya alikuwa amenawa mpira wakati wa shambulio hilo.

Stars ilisawazisha 1-1 kupitia kwa mchezaji matata wa Bandari FC Abdallah Hassan dakika ya 65 baada ya msongamano katika lango la Misri.

Kenya ilipata pigo jingine dakika ya 76 wakati Johnstone Omurwa alionyeshwa kadi nyekundu kwa kuchezea vibaya Mostafa Mohamed.

Kenya inaungana na Togo nje ya safari ya kufika Cameroon kwa dimba la AFCON litakalofanyika mwaka 2022 nazo Misri na Comoros zimefuzu kutoka kundi hili. Togo ilitoka 0-0 dhidi ya wenyeji Comoros mapema Alhamisi na kusalia na alama mbili, huku wanavisiwa hao wakitinga AFCON kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Comoros, ambayo itazuru Misri kwa mchuano wake wa mwisho hapo Machi 29, ilijikatia tiketi kwa kufikisha alama tisa dhidi ya Kenya ambayo sasa ina alama nne. Kenya na Togo zitakutana jijini Lome mnamo Machi 29 katika mechi itakayoamua nani kati yao atavuta mkia. Kenya ina alama tatu.

Sudan, ambayo iko katika Kundi C, ilizaba Sao Tome & Principe 2-0 katika taifa hilo la Afrika ya Kati, na kufikisha alama tisa katika nafasi ya tatu nyuma ya Ghana na Afrika Kusini kwa tofauti ya ubora wa magoli. Itaalika Bafana Bafana kwa mechi yake ya mwisho mnamo Machi 28 kuamua nani kati yao atakuwa shabiki 2022 na nani ataelekea Cameroon.

Ethiopia ililipua wanavisiwa wa Madagascar 4-0 mjini Bahir Dar katika mechi ya Kundi K kupitia mabao ya Amanuel Gebremichael, Getaneh Kebede, Abubeker Nassir na Shimelis Bekele. Walia ibex wanaongoza kundi lao kwa alama tisa wakiwa wamesakata mchuano mmoja zaidi dhidi ya Ivory Coast na Niger zitakazocheza mechi yao ya tano hapo Machi 26. Ivory Coast, ambayo itaalika Ethiopia katika mechi yake ya mwisho Machi 30, ina alama saba, sawa na Madagascar. Niger inavuta mkia kwa alama tatu.

Rwanda ilipepeta Msumbiji 1-0 kupitia bao la Lague Byiringiro jijini Kigali. Ushindi huo wa kwanza wa Amavubi Stars uliweka timu hiyo katika nafasi ya pili kwa alama tano, moja mbele ya Msumbiji na Cape Verde itakayomenyana na Cameroon hapo Machi 26. Mechi ya mwisho ya Rwanda itakuwa dhidi ya Indomitable Lions nchini Cameroon mnamo Machi 30. Cameroon iko juu ya jedwali kwa alama 10.

Uganda ilitoka 0-0 dhidi ya viongozi wa Kundi B Burkina Faso mnamo Jumatano kwa hivyo inahitaji sare ama ushindi dhidi ya Malawi ugenini ifuzu. Itaingia mchuano huo wa Machi 29 na presha kwa sababu timu hizo zimeachana kwa alama moja pekee. Cranes ina alama nane nayo Flames ni ya tatu kwa alama saba. Sudan Kusini iki mkiani kwa alama tatu na imeshaaga kampeni ya kuelekea Cameroon mwaka 2022.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Hofu kuhusu chanjo itatuliwe

Watu 26 wafariki kwa corona