• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Harry Kane haondoki Spurs – kocha Nuno Espirito

Harry Kane haondoki Spurs – kocha Nuno Espirito

Na MASHIRIKA

KOCHA mpya wa Tottenham Hotspur, Nuno Espirito Santo, amesisitiza kuwa mshambuliaji na nahodha Harry Kane “bado ni mchezaji wao” huku akiahidi kuzungumza kwa kina na mwanasoka huyo raia wa Uingereza pindi atakaporejea kambini.

Kane, 27, kwa sasa angali likizoni baada ya kuongoza Uingereza kutinga fainali ya Euro iliyowakutanisha na Italia mnamo Julai 11 uwanjani Wembley.

Kwa mujibu wa vyombo vingi vya habari nchini Uingereza, Kane ana maagano na Spurs kwamba angejiengua kambini mwa kikosi hicho mwishoni mwa msimu wa 2020-21. Matamanio yake ni kutua kambini mwa Manchester City japo Real Madrid ya Uhispania pia inahemea maarifa yake.

“Kwa sasa anahitaji muda wa kupumzika na kujiandaa kwa msimu mpya. Baada ya hapo, tutashiriki kikao kirefu na kuzungumza kwa kina,” akasema Nuno ambaye ni raia wa Ureno.

“Kane ni mchezaji wetu. Hilo ni suala lisilo na ubishi. Tunatazamia kuendelea kujivunia huduma zake kwa misimu kadhaa ijayo. Ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa na takwimu zinaonyesha,” akaongeza kwa kuthibitisha kwamba fowadi Gareth Bale hatakuwa tena sehemu ya kikosi cha Spurs baada ya mkopo wake kutoka Real Madrid kukamilika.

“Hatakuwa sehemu ya kikosi chetu. Nadhani atarejea Real kwa kuwa angali na mkataba nao,” akasema Nuno kumhusu nyota huyo raia wa Wales mwenye umri wa miaka 32.

Kufikia sasa, Man-City wako radhi kuweka mezani kima cha Sh15.6 bilioni kwa ajili ya Kane ambaye kocha Pep Guardiola anahisi kwamba atakuwa kizibo maridhawa cha Sergio Aguero aliyeyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona.

Kabla ya kumshawishi Nuno kujiunga nao, Spurs walipitia kipindi kigumu cha kutafuta kocha mrithi wa Jose Mourinho aliyetimuliwa mnamo Aprili 19, 2021.

Antonio Conte, Paulo Fonseca, Gennaro Gattuso na kocha wa zamani Mauricio Pochettino ni miongoni mwa wakufunzi waliokuwa wakihusishwa pakubwa na Spurs baada ya kuondoka kwa Mourinho ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya AS Roma nchini Italia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Kipa Scherpen aingia katika sajili rasmi ya Brighton

Waiguru ahisi huu ni wakati mwafaka wa Jubilee kuzinduka