• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Hatimaye Ozil aondoka Arsenal

Hatimaye Ozil aondoka Arsenal

Na MASHIRIKA

MESUT Ozil, 32, amewaaga wanasoka wenzake kambini mwa Arsenal huku akitarajiwa sasa kuingia katika sajili rasmi ya Fenerbahce jijini Istanbul, Uturuki.

Nyota huyo mzaliwa wa Uturuki na raia wa Ujerumani ameafikiana na vinara wa Arsenal watamatishe mkataba wake uwanjani Emirates. Kwa mujibu wa ripoti, Ozil atapokezwa kitita cha Sh980 milioni – mshahara aliokuwa apokezwe hadi wakati ambapo kandarasi yake ingekamilika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Ozil ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia ana kiu ya kurejea ugani kusakata soka baada ya kocha Mikel Arteta kumtema kwenye kikosi cha Arsenal kuanzia Machi 2020.

Erkut Sogut ambaye ni wakala wa Ozil, amethibitisha kwamba wameafikiana na mkurugenzi wa kiufundi wa Arsenal, Edu Gaspar kufanikisha uhamisho wa sogora huyo hadi Fenerbahce bila ada yoyote.

Kulingana na gazeti la Sunsport, Ozil amekubali kupunguziwa sehemu ya mshahara aliokuwa apokezwe na Arsenal hadi mwishoni mwa msimu huu ili “aondoke ugani Emirates kwa uzuri”.

Mnamo Januari 16, mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid aliwapa baadhi ya wachezaji wenzake ujumbe wake wa mwisho baada ya kushiriki kipindi cha mazoezi uwanjani London Colney.

Awali, Ozil alikuwa amesema, “Nililelewa Ujerumani nikiwa shabiki mkubwa wa Fenerbahce. Hicho ni kikosi ambacho naweza kulinganisha na Real Madrid nchini Uhispania. Ndiyo klabu kubwa na maarufu zaidi nchini Uturuki.”

Ozil ndiye mchezaji wa Arsenal anayejivunia mafanikio makubwa zaidi ugani Emirates baada ya kunyanyua mataji manne ya Kombe la FA katika kipindi cha miaka saba na nusu tangu abanduke kambini mwa Real kwa kima cha Sh5.9 bilioni.

Ozil aliweka historia ya kuwa mchezaji anayedumishwa kwa mshahara mkubwa zaidi uwanjani Emirates baada ya kutia saini mkataba mpya uliomshuhudia akipokezwa Sh49 milioni kwa wiki kuanzia Disemba 2018.

Hata hivyo, hajawahi kuwajibikia Arsenal msimu huu baada ya kutupwa nje ya kikosi kinachotegemewa na Arteta kwenye kivumbi cha EPL na Europa League.

Hadi kufikia sasa, Ozil amechezeshwa na Arsenal mara 254 na ameifungia klabu hiyo mabao 44 na kuchangia 77 mengine.

“Ozil yuko pua na mdomo kuingia kambini mwetu. Ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye uwezo wake umethibitishwa. Amechangia takriban mabao yote ambayo yamefungwa katika kila mechi na vikosi alivyowahi kuchezea,” akasema mkurugenzi wa michezo kambini mwa Fenerbahce, Emre Belozoglu.

Tetesi za Ozil kujiunga na Fenerbahce zilianzishwa na mwanasoka huyo mwenyewe baada ya kupakia kwenye mtandao wake wa Twitter picha yake akiwa jijini Istanbul. Chini ya picha hiyo, aliandika: “Huu mji…#throback #Istanbul.”

Ozil alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia timu ya taifa ya Ujerumani ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil baada ya kuwazidi nguvu Argentina kwenye fainali.

Kwa mujibu wa gazeti la Fanatik nchini Uturuki, Ali Koc ambaye ni mwenyekiti wa Fenerbahce angali jijini London, Uingereza kukamilisha uhamisho wa Ozil aliyehusishwa pia na uwezekano mkubwa wa kujiunga na kikosi cha DC United nchini Amerika.

Mchuano wa mwisho kwa Ozil kambini mwa Arsenal ni mechi iliyoshuhudia kikosi cha Arteta kikisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya West Ham United mnamo Machi 7, 2020.

Ozil hakusajiliwa na Arsenal kwa minajili ya kampeni za msimu huu wa 2020-21 katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Europa League.

 “Kumekuwapo na changamoto tele. Lakini sijawahi kujutia maamuzi yangu ya kujiunga na Arsenal. Nimejivunia muda wangu kambini mwa kikosi hicho japo mambo yalibadilika ghafla baada ya janga la corona kubisha,” akatanguliza Ozil.

“Zipo nchi mbili ambazo ningependa sana kuchezea ligi zao kabla ya kustaafu ulingoni. Amerika na Uturuki,” akaongeza Ozil.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sababu za kudhibiti filamu wanazotazama watoto

PSG warejea kileleni mwa jedwali l