Na GEOFFREY ANENE

MASHINDANO ya masumbwi ya Bara Afrika ya ukanda wa tatu yanang’oa nanga baadaye Jumatatu jijini Kinshasa yakileta pamoja mataifa 11 ikiwemo Hit Squad ya Kenya.

Hit Squad iliondoka jijini Nairobi mapema Jumapili na kuwasili siku hiyo ikiwa na mabondia 16.

Vijana wa kocha Benjamin Musa wameamkia Jumatatu kupimwa uzani kuhakikisha hawako chini wala kupitisha uzani unaotarajiwa.

Musa ameeleza Taifa Leo kuwa droo ya mapigano yatafanywa leo Jumatatu kabla ya mabondia kuanza kujibwaga ulingoni.

Nick Okoth, Christine Ongare, Elly Ajowi na Elizabeth Akinyi, ambao wamefuzu kuwakilisha Kenya katika Michezo ya Olimpiki mwezi Julai/Agosti jijini Tokyo nchini Japan, ni baadhi ya mabondia Wakenya ambao wako DR Congo.

Mbali na Kenya kutafuta ubingwa wa mashindano hayo, mabondia wanaoenda Olimpiki watatumia mapigano kujipima nguvu na kujiimarisha.

Mataifa yatakayoshiriki ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (wenyeji), Kenya, Uganda, Burundi, Cameroon, Congo Brazzaville, Equatorial Guinea, Gabon, Msumbiji, Morocco na Libya.