• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Cyrus Ruru afariki na kuacha maswali kuhusu kifo cha diwani 2012

Cyrus Ruru afariki na kuacha maswali kuhusu kifo cha diwani 2012

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Baraza la Mji wa Maragua katika Kaunti ya Murang’a Bw Cyrus Ruru Mwaura alifariki na kutamatisha maisha yake yaliyojaa utata mwingi katika eneo hilo.

Bw Ruru akisifiwa na wengi kama mwanasiasa shupavu aliyekuwa na uwezo wa kujipenyeza katika dili za kisiasa na za kumfaa kiuchumi aliishia kwa wakati mmoja kuhusishwa na kifo cha diwani mwenza wa Muthithi Bw Charles Obed Thuo ambaye aliaga dunia Agosti 2012.

Kinaya ni kuwa, Bw Ruru alitajwa kama aliyekuwa amezama ndani ya imani ya Kikristo ambapo katika kanisa la AIPCA, alikuwa mwenyekiti wa Dayosisi ya Maragua na pia mwekahazina katika bodi ya kitaifa.

Bi Sabina Chege akiwa ni mbunge mwanamke mwakilishi wa Kaunti ya Murang’a akimtaja mwendazake kama “rafiki yangu wa dhati na mshauri wa kisiasa” na ambaye Februari 14 iliyopita alimsaidia katika hafla ya kuchanga pesa za kanisa moja eneo hilo.

Bw Thuo alijulikana kwa jina la majazi la Wathu na alikuwa amefanya kazi kama meneja katika mashamba kadha ya biashara za kilimo kabla ya kurejea nyumbani na kuwekeza katika biashara ya mauzo ya vitabu na vifaa vingine vya kutumika shuleni.

Aidha, alikuwa mkulima hodari lakini akiwa na vituko kadha vya kijamii ambavyo vingehatarisha maisha yake kupitia kuvutia maadui kadha.

Katika kisa hicho, Bw Thuo alikabiliwa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki na silaha butu na wakamshambulia na kumwibia.

Alishambuliwa kwa vifaa butu na wahalifu wakihepa, walipiga risasi angani ili kuogofya wanakijiji ambao walikuwa wameanza kujitokeza katika kisa hicho cha mwendo wa saa mbili usiku.

Ni tukio lililovuruga siasa za eneobunge la Kigumo kwa kiwango kikuu ikizingatiwa kuwa Bw Thuo alikuwa ametangaza nia ya kuwania ubunge wa Kigumo.

Katika uchunguzi uliofuatia, meneja wa Bw Ruru alinaswa akiwa na simu ya mkononi ya Bw Thuo na ambayo ilikuwa imeibwa kutoka kwa nyumba ya marehemu siku aliyoshambuliwa na akaaga dunia akitibiwa katika hospitali ya Maragua.

Kuna kofia aina ya godfather ambayo ilinaswa ikiwa na kijana wa mwanasiasa mwingine wa Kaunti ya Murang’a na ambaye aliishia kuwa diwani katika uchaguzi mkuu wa 2013 lakini akatimuliwa na wapigakura katika uchaguzi wa 2017.

Vile vile, Bw Ruru wakati huo akiwa diwani wa wadi ya Ng’araria katika kaunti ndogo ya Kandara alirithi cheo cha Bw Wathu cha uenyekiti wa Baraza la Mji wa Maragua.

Ni kisa ambacho kilijiangazia kwa kiwango kikuu kama kilichopangwa kisiasa huku jina la Bw Ruru likikataa kuondoka kutoka orodha ya waliokuwa na habari muhimu lakini ambazo hadi sasa zimeyeyuka kama hewa yabisi na ataendelea kutulia nazo kaburini.

Bw Ruru hakukamatwa na hakuhojiwa, na ingawa kuna kesi ziliandaliwa katika mahakama ya Kigumo na zikaamuliwa, wenyeji hasa katika kijiji cha Kihingo alikokuwa na boma mwendazake Bw Thuo, hawajawahi kuridhika kuwa wapangaji wa njama hiyo chafu ya mauaji hayo waliwahi kukamatwa bali waliokuwa tu vibarua katika unyama huo ndio walinaswa.

Kuna baadhi walihisi kuwa Bw Wathu alikuwa amelengwa kwa kuwa mwadilifu na aliyekataa katakata mashamba ya umma eneo hilo yaibwe na mitandao ya matapeli ndani ya vyeo vya kisiasa na “ni lazima angefyekwa aondoke kutoka afisini.”

Wengine walisema kuwa Bw Wathu aliingia katika hatari ya maisha yake kwa kutangaza nia ya kuwania ubunge wa Kigumo na ambapo alisafiri pamoja na wanasiasa wengine hadi Ichaweri kukutana na Uhuru Kenyatta mwaka wa 2012 wakati wakisuka chama cha The National Alliance (TNA).

Yapo madai kuwa Bw Wathu baadaye alirejea katika mkutano na wandani wengine wa TNA na ambapo alijipendekeza kama aliyekuwa mfaafu zaidi wa kuaminiwa kupigia debe chama hicho kilichokuwa kipya na kisha awanie ubunge wa Kigumo.

Ni hali ambayo inasemwa kuwa ilikemewa vikali na Bw Ruru kwa niaba ya wengine waliokuwa na ushawishi katika siasa za eneo hilo la Kigumo na Murang’a kwa ujumla na ndio kumkata miguu, ikapangwa jinsi ambavyo angeondoka afisini na kwa uhai ndipo marafiki wa mitandao ya unyakuzi wapate mwanya wa kutekeleza miradi yao bila shinikizo za kupingwa na Bw Thuo.

Kwa sasa, Bw Ruru akiwa ni marehemu, na katika ile hali ya kwamba njia ya mhini na mhiniwa huwa ni moja, waliojitokeza kutoa rambirambi zao walimtaja kama mwanasiasa na mfanyabiashara shupavu aliyekuwa amefanikiwa kujikusanyia ploti kadha katika maeneo ya Kenol na Thika.

Kabla ya kuaga dunia, Bw Ruru alikuwa amekodisha jengo lake lililo katika mji wa Kenol kwa waanzilishi wa hospitali mpya ya upasuaji ya Santamore kwa kitita kilichotajwa tu kuwa ni “kitamu.”

Habari kutoka kwa familia hazikufichua kiini cha mauti ya Bw Ruru, ikisema tu “ni ukweli ametuacha na habari zaidi zitatolewa baadaye.”

Bw James Maina ambaye alikuwa akifanya kazi na Bw Ruru alimtaja kama “shujaa, mkarimu na aliyekuwa na ubunifu wa kipekee katika kusaka dili za kumpa ukwasi.”

Bw Maina anasema kuwa Bw Ruru alikuwa mcheshi kwa njia ya kipekee na alipenda sana ushirika tu wa wale ambao wangemfaa kuboresha maisha yake kupitia kufurisha mkoba wake ujae pesa.

Ni masikitiko makuu kuwa Bw Ruru hakuandika kitabu cha kuelezea maisha yake ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ili kuweka wazi shaka nyingi ambazo zilikumba uhai wake.

You can share this post!

Hit Squad yasubiri droo kabla ya mapigano ya mataifa 11...

Ole Kina na Buzeki kujiunga na ANC, adokeza Malala