• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Papa Francis aunga kuondolewa kwa ulinzi wa hakimiliki za uvumbuzi wa chanjo ya corona

Papa Francis aunga kuondolewa kwa ulinzi wa hakimiliki za uvumbuzi wa chanjo ya corona

Na MASHIRIKA

VATICAN CITY, Holy See

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis Jumamosi aliunga mkono wito wa kuondolewa usiri wa hakimiliki (patent rights) ya utengenezaji chanjo ya corona ili kuziwezesha nchi maskini kupata chanjo hiyo kwa urahisi.

Kwenye taarifa iliyonakiliwa kwa lugha ya Kihispania, Papa huyo alikosoa mataifa yanayohodhi chanjo hiyo badala ya kusambaza kwa mataifa mengine “yanayoteseka.”

“Sera ya kutosambaza nje chanjo ni sawa na aina nyingine hatari ya virusi. Aina nyingine ya virusi ni sheria za kibiashara za hakimiliki ambazo zimezingatiwa zaidi badala ya kanuni za upendo na afya ya binadamu,” Papa Francis akaeleza.

Kauli ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki imejiri baada ya Amerika kutangaza kuwa inaunga mkono kuondolewa kwa hakimiliki iliyowekwa na kampuni za kutengeneza chanjo ya Covid-19 ili kuimarisha utengenezaji chanjo.

Hatua hiyo hata hivyo ilipingwa vikali na kampuni za kutengeneza dawa kwa sababu itaathiri ubunifu wao siku za usoni. Zinashikilia kuwa hatua hiyo haitaimarisha uzalishaji chanjo ya Covid-19 kwa wingi.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Huenda Clarke Oduor akajiengua Barnsley iliyomfanya shabiki...

Neymar sasa kuchezea PSG hadi 2025