• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ivory Coast na Morocco wajikatia tiketi za kushiriki fainali za AFCON 2022

Ivory Coast na Morocco wajikatia tiketi za kushiriki fainali za AFCON 2022

Na MASHIRIKA

USHINDI wa 3-0 uliosajiliwa na Ivory Coast dhidi ya Niger uliwakatia tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon mnamo 2022.

Mabao ya Ivory Coast ambao sasa wanaongoza Kundi K, yalipachikwa wavuni na Serge Aurier, Max Gradel na Wilfried Kanon.

Katika Kundi F, Cape Verde walitoka nyuma na kuduwaza Cameroon kwa kichapo cha 3-1. Pierre Kunde aliwaweka Cameroon kifua mbele kabla ya Kuca, Ryan Mendes na Macky Bagnack aliyejifunga kuwapa Cape Verde mabao matatu.

Katika Kundi I, Congo waliambulia sare tasa dhidi ya Senegal. Congo kwa sasa wanahitaji alama moja pekee katika mechi ya mwisho itakayowakutanisha na Guinea-Bissau mnamo Machi 30 ili kujipa tiketi ya kutua Cameroon mnamo Januari 2022.

Licha ya kuambulia sare tasa dhidi ya Mauritania, Morocco walifuzu. Hii ni baada ya Burundi kutoka nyuma na kuwalazimishia Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) sare ya 2-2 jijini Bujumbura.

Mabao ya CAR yalipachikwa wavuni na Louis Mafouta huku Burundi wakifunga yao kupitia Saidi Ntibazonkiza na Christophe Nduwarugira. CAR sasa wana ulazima wa kushinda Mauritania katika mechi yao ya mwisho ili kufuzu.

Katika mchuano mwingine wa Jumamosi, Guinea-Bissau waliwachapa Swaziland 3-1 mjini Lobamba na kuweka hai matumaini finyu ya kufuzu kutoka Kundi I linalojumuisha pia Congo na Senegal ambao tayari wamefuzu.

Marcelo Djalo aliwaweka Guinea-Bissau uongozini baada ya 15 kabla ya Felix Badenhorst kusawazisha mambo dakika nne baadaye. Alfa Samedo na Pele walifunga mabao mawili zaidi ya Guinea-Bissau kunako dakika za 24 na 50 mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ronaldo ashindwa kutambisha Ureno dhidi ya Serbia

Super Eagles ya Nigeria yapiga Benin na kufuzu kwa fainali...