• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Jagina Pele, aliyewahi kuzuru Kenya, atazikwa Jumanne

Jagina Pele, aliyewahi kuzuru Kenya, atazikwa Jumanne

NA MASHIRIKA

RIO DE JANEIRO, BRAZIL

JAGINA wa soka duniani, Pele, atazikwa siku ya Jumanne jijini Sao Paulo baada ya maombolezo ya siku tatu nchini mwake Brazil kufuatia kifo chake Alhamisi akiwa na umri wa miaka 82.

Mshambulizi huyo wa zamani na mchezaji wa pekee katika historia kutwaa Kombe la Dunia mara tatu, aliaga dunia katika hospitali ya Albert Einstein mjini Sao Paulo, Brazil, baada ya kuugua saratani ya utumbo mpana kwa muda mrefu.

Pele ni mfungaji bora wa mabao wa timu ya taifa ya Brazil akiwa amecheka na nyavu za upinzani mara 77 katika mechi 92.

Akitambulika kwa jina rasmi kama Edson Arantes do Nascimento, alijizolea umaarufu aliposhinda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1958 baada ya kufunga magoli mawili katika fainali dhidi ya wenyeji Uswidi.

Mwanawe wa kike Kely Nascimento, ambaye amekuwa akitoa taarifa za punde kuhusu afya ya babake kutoka hospitalini.

Ndiye alitangaza kukata roho kwa jagina huyo kwenye mtandao wa Instagram siku ya Alhamisi.

“Kila kitu tumekuwa ni kwa sababu yako. Tunakupenda bila kikomo. Lala mahali pema peponi,” ulisema ujumbe huo ukiandamana na picha ya Pele na wanawe wameshikana mikono.

Serikali ya Brazil ilitangaza siku tatu za kuomboleza Pele.

Supastaa huyo alizaliwa katika familia maskini mjini Sao Paulo. Talanta ya kusakata kabumbu ndiyo ilikuwa kismati yake maishani huku akiishia kushinda Kombe la Dunia mwaka 1958, 1962 na 1970.

Mnamo 1976 jagina huyo alizuru Kenya na kujumuika na wanafunzi wa shule ya upili mjini Nairobi, katika mradi wa kampuni maarufu ya soda wakati huo, Pepsi, wa warsha za soka kukuza kandanda miongoni mwa vijana.

Ujumbe uliochapishwa katika ukurasa rasmi wa Pele kwenye mtandao wa Twitter ulisema mnamo Alhamisi: “Motisha na upendo ni vitu Mfalme Pele alifahamika navyo. Aliaga dunia kwa amani leo. Upendo, upendo na upendo, milele.”

  • Tags

You can share this post!

Huyu ‘Iniesta’ wa Nzoia ni hatari kwa pasi za maangamizi

Kesha marufuku Lamu kwa kuhofia usalama

T L